
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amesema kuwa shirika linatumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kama jukwaa la kuonesha huduma na teknolojia zinazochochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Akizungumza Julai 4, 2026, baada ya kutembelea banda la TTCL katika maonesho hayo, Marwa ameeleza kuwa shirika linaendelea kutoa huduma za intaneti ya kasi ya juu kwa gharama nafuu, kwa lengo la kuboresha mawasiliano na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.
Amebainisha kuwa huduma zinazooneshwa ni pamoja na Sifa Soni, FTTx Experience Centre na National ICT Data Centre (NIDC), ikiwemo huduma za cloud computing zinazowawezesha wateja kuhifadhi taarifa zao kwa usalama bila kuhitaji uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kuhifadhi data.
Akizungumzia utendaji wa shirika, Marwa amesema TTCL ilipata faida ya takribani shilingi bilioni 23 katika mwaka wa fedha 2024/25, na inatarajia kuongeza kiwango hicho katika mwaka wa fedha 2025/26 kutokana na ongezeko la mapato na wigo mpana wa wateja.
Aidha, amesisitiza kuwa TTCL itaendelea kuboresha huduma zake, kupanua wigo wa huduma na kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.









