
Serikali imeipongeza Azania Group kwa kutimiza miaka 25 ya mafanikio katika sekta ya viwanda na biashara, huku ikieleza kuwa kampuni hiyo imeendelea kuwa mfano wa uwekezaji wa wazawa baada ya kutangaza mpango wa kuwekeza zaidi ya Shilingi trilioni moja katika miradi mbalimbali ya uzalishaji nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), wakati akizindua maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Azania Group yaliyofanyika Agosti 1, 2026, katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Kapinga amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa mshirika muhimu wa Serikali katika utekelezaji wa agenda ya uchumi wa viwanda.
Aidha, ukuaji wa uwekezaji huo unaonesha imani kubwa ya sekta binafsi katika uchumi wa Tanzania na utaongeza ajira, kukuza uzalishaji wa viwandani, kuinua kipato cha wakulima na kuongeza mapato ya Serikali.

Kwa kipindi cha robo karne, Azania Group imejijengea rekodi ya mafanikio kupitia uwekezaji katika viwanda, uongezaji wa thamani ya malighafi za ndani, utoaji wa maelfu ya ajira na mchango mkubwa katika mapato ya Serikali kupitia kodi.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuimarisha miundombinu ya reli ya kisasa ya SGR, bandari, barabara, nishati na TEHAMA, hatua ambazo zimepunguza gharama za uzalishaji na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uzalishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
Kapinga amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuharakisha maendeleo ya viwanda na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Hivyo, amewataka wawekezaji kuendelea kuwekeza katika teknolojia, tafiti na ubunifu ili kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kuifanya Tanzania kufikia azma ya kuwa uchumi wa dola trilioni moja.
Hata hivyo, Waziri Kapinga ameipongeza Azania Group kwa mafanikio ya miaka 25 na kueleza kuwa uwekezaji mpya wa zaidi ya Shilingi trilioni moja ni hatua muhimu itakayochochea ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa Taifa.









