Home Kitaifa TRA NA TFF WAINGIA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO

TRA NA TFF WAINGIA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeingia Makubaliano ya Ushirikiano na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwaajili ya kushirikiana kuhamasisha ulipaji Kodi wa hiari.

Akizungumza baada ya kuingia Makubaliano hayo Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema wameingia Makubaliano hayo ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan la kutaka Mifumo ya Taasisi za Serikali isomane.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema Makubaliano waliyoingia yanakwenda kuisaidia nchi maana watashirikiana kutoa Elimu ya Kodi kwa wachezaji na mashabiki wa mpira wa miguu na pia wataweza kubadilishana taarifa jambo ambalo linatarajiwa kuwa na tija katika ukusanyaji wa Kodi.

Tumekubaliana tutashirikiana na TFF kuhamasisha ulipaji Kodi wa hiari nchini na tunatambua kuwa mpira wa miguu una mashabiki wengi hivyo tukitumia jukwaa hili ujumbe wa nchi wa Kodi kuhusu ulipaji Kodi wa hiari utawafikia watu wengi zaidi “ amesema Mwenda.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema upo uhusiano mkubwa baina ya Kodi na Mpira wa miguu maana Viwanja vinavyotumika ni matokeo ya Kodi na hata Akademia za michezo zilizopo Tanga na Kigamboni zimejengwa kutokana na Kodi hivyo ili nchi iendelee kupiga hatua na kuwa na mazingira mazuri ya michezo ni lazima watu waendelee kulipa Kodi kwa hiari.

Kwa upande wake Rais wa TFF Bw. Wallace Karia amesema mkataba waliosaini ni wa miaka mitatu lakini jambo la ushirikiano wa kutoa Elimu ya kulipa Kodi kwa hiari ni endelevu na litaendelea kufanyika hata baada ya hiyo miaka mitatu kwa ustawi wa nchi.

Karia amesema Viwanja vyote vya Mpira wa miguu vinavyomilikiwa na TFF mkoani na wilayani vitapambwa na jumbe za Kodi zikihamasisha ulipaji Kodi wa hiari na kueleza umuhimu wa kulipa Kodi kwa maendeleo ya nchi na ustawi wa michezo nchini.

Hakuna Kodi hakuna Chani, hakuna Kodi hakuna Afcon, hakuna Kodi hakuna Ligi Kuu, hakuna Kodi hakuna Goli la Mama” amesema Karia.

Katika hatua nyingine amewaagiza viongozi wa vyama vya Mpira wa Miguu mikoa na wilaya zote nchini, kushirikiana na TRA kuhakikisha ujumbe wa Kodi unawafikia wachezaji, mashabiki na wadau wa michezo katika maeneo yao.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!