Home Kimataifa TANZANIA NA SINGAPORE KUBADILISHANA WAKUFUNZI KWENYE VYUO VYA UFUNDI NA UJUZI

TANZANIA NA SINGAPORE KUBADILISHANA WAKUFUNZI KWENYE VYUO VYA UFUNDI NA UJUZI

Na Mathias Canal, WEST-Dar es salaam

Serikali imesema kuwa Tanzania ipo tayari kubadilishana na Singapore wakufunzi wa vyuo vya Ufundi na Ujuzi ili kuongeza uelewa zaidi kwa wanafunzi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 2 Agosti 2022 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Singapore nchini Tanzania Mhe. Douglas Foo Jijini Dar es salaam.

Waziri Mkenda amesema kuwa wakufunzi wa Tanzania wataenda nchini Singapore kujifunza namna nchi hiyo ilivyofanikiwa katika ufundi na elimu ujuzi, vilevile wakufunzi wa Singapore kutembelea vyuo vya ufundi na elimu ujuzi nchini Tanzania.

Amesema kwa pamoja wakufunzi hao watakapozuru katika nchi hizo watajadiliana kwa pamoja namna bora ya kuimarisha elimu ujuzi, ambapo amebainisha kuwa Tanzania itanufaika zaidi kwa wataalamu wa Singapore kwani nchi hiyo imefanikiwa zaidi katika sekta ya elimu ujuzi.

“Tunapoenda huko mbele elimu ya ujuzi ni lazima ipate kipaumbele kikubwa ili wanafunzi wanapomaliza iwe rahisi kujiajiri na kujipatia kipato iikiwa ni pamoja na kuweza kubadilisha maisha yao ikiwemo kuajiri watu wengine” Amekariri Waziri Mkenda

Katika Mazungumzo hayo, Waziri Mkenda amemuhakikishia Balozi huyo kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Singapore katika sekta ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Kwa Upande wake Balozi wa Singapore nchini Tanzania Mheshimiwa Douglas Foo amesema Singapore inatarajia kuongeza ushirikiano na Tanzania katika sekta ya elimu.

Pia Amesema Singapore imeendelea na uwekezaji katika teknolojia unaorahisisha ufanyaji kazi pamoja na ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya kielimu hivyo imeridhia kuunganisha uelewa wa pamoja wa wakufunzi wa ufundi na elimu ujuzi.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!