Home Kitaifa TANGA YAENDELEA KUPAA: RAIS SAMIA AZINDUA SHULE YA WASICHANA NA MIRADI MINGINE

TANGA YAENDELEA KUPAA: RAIS SAMIA AZINDUA SHULE YA WASICHANA NA MIRADI MINGINE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumanne, Februari 25, 2025, anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Tanga kwa siku ya tatu. Katika ratiba yake, anatarajiwa kuzindua Shule ya Sekondari ya Wasichana Tanga na baadaye kutembelea na kuzindua Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, pamoja na kuzungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali.

Rais Samia pia atazindua Jengo la Halmashauri ya Mji wa Handeni, ambalo limegharimu Shilingi bilioni 4.2. Jengo hilo linajumuisha hoteli, kumbi za mikutano, na sehemu za kukodisha kwa taasisi za kifedha, likilenga kuboresha huduma za kiutawala na kijamii katika mji huo.

Aidha, ataweka jiwe la msingi na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji wa Miji 28 uliopo mtaa wa Vibaoni, wilayani Handeni. Mradi huu ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji safi na salama.

Shule ya Sekondari ya Wasichana Tanga ilitengewa bajeti ya takribani Shilingi bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wake. Lengo ni kuboresha mazingira ya elimu kwa wasichana na kuwahamasisha kusoma masomo ya Sayansi ili kuongeza ushiriki wao katika sekta hiyo muhimu.

Ziara hii ni ya kwanza kwa Rais Samia tangu awe madarakani, ikiwa na lengo la kufuatilia thamani ya fedha na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayogharimu zaidi ya Shilingi trilioni 3.1. Serikali inaendelea kusisitiza uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali kwa manufaa ya wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!