Home Kitaifa MILIONI 870 KUSAMBAZA MAJI YA BOMBA VIJIJI VYA SEKA NA KABONI JIMBO...

MILIONI 870 KUSAMBAZA MAJI YA BOMBA VIJIJI VYA SEKA NA KABONI JIMBO LA MUSOMA VIJIJINI

Na Shomari Binda-Musoma

JUMLA ya shilingi milioni 870 zimetolewa na serikali kwaajili ya usambazaji maji ya bomba kwenye vijiji vya Seka na Kaboni vilivyopo Kata ya Nyamrindirira jimbo la Musoma vijijini.

Jana februari 24/2025 Wakala wa Huduma ya Usambazaji Maji Vijijini ( RUWASA) Wilaya ya Musoma ilisainiana mkataba na kumkabidhi mkandarasi anayetekeleza mradi wa usambazaji maji kwenye vijiji hivyo ukishuhudiwa na mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo meneja wa RUWASA wa Wilaya hiyo Edward Sironga amesema mkataba huo unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 6.

Amesema sehemu ya mkataba huo ni usambazaji wa mabomba na baadae kuwaunganishia maji wananchi kwenye makazi yao.

Sironga amesema watamsimamia mkandarasi kwa karibu kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na wananchi wanaunganishiwa maji.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka akizungumza kwenye makabidhiano hayo amesema ataufatilia mradi huo kuona ndani ya kipindi hicho cha miezi 6 unakamilishwa.

Amesema lengo la serikali kutoa fedha nyingi za miradi ya maji ni kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kumtua mama ndoo kichwani.

Chikoka amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaangalia wananchi kwa kutoa fedha za miradii ikiwemo ya maji.

Mkuu huyo wa Wilaya amemshukuru pia mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo kwa ufatiliaji wake wa miradi na kuhakikisha inafika jimboni.

Kwa upande wao wananchi wa Kijiji cha Seka wametoa shukrani zao kwa Rais Samia na mbunge wao kuwafikishia maji ambayo yanakwenda kuondoa kero waliyokuwa nayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!