
Na Beatrice Sanga-MAELEZO
Serikali kupitia Ofisi ya Hazina imesema itahakikisha kila Shirika au Taasisi iliyopo chini ya ofisi yake inazalisha kwa ufanisi na kuongeza mapato ama gawio kwa serikali ili kuinua uchumi wa watanzania.
Hayo yameelezwa July 13, 2023 na Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu, wakati wa mkutano uliowakutanisha ofisi ya Msajili wa Hazina, Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) Jukwaa la Wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wenye malengo ya kueleza shughuli mbalimbali zinazofanywa na benki hiyo kwaajili ya maendeleo ya wakulima nchini.

Mchechu amebainisha kuwa kazi aliyopewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusimamia mabadiliko na utendaji kazi wa Taasisi na Mashirika hayo yanafanyika.
“Tunatamani Taasisi za umma zifanye kazi kama sekta binafsi, hatuna haja ya kuchukua watu kutoka taasisi binafsi halafu waje huku washindwe, lakini wanaweza wakashindwa kwasababu, kwanza hatujatengeneza mazingira mazuri, hatujawawezesha lakini pia hatuna utamaduni wa kupima utendaji kazi wala kuwajibishana.” Amesema Mchechu.
Mchechu amebainisha kuwa mabadiliko yanayoendelea, watazingatia mambo mengi katika utendaji kazi wa mtu mmoja mmoja na matokeo anayochangia kupitia ofisi aliyopo.
“Katika mabadiliko tunayoyafanya tutakuwa na utaratibu wa kupimana utendaji kazi, kupeana malengo, lakini pia kuhakikisha tuna watu sahihi wanaoenda kuziongoza hizo Taasisi, lakini pia kuwaachia uhuru wa uwajibikaji na kuwawezesha kwa rasilimali ili waweze kufanya kazi zao, malengo ni kuongeza mchango wa Taasisi hizi katika Pato la Taifa kwa ujumla.” Amefafanua Mchechu.
Aidha amesema kuwa kwa sasa wako kwenye mchakato wa kupitia utendaji kazi wa Taasisi na Mashirika mbalimbali ya umma ambayo yako chini ya ofisi ya Msajili wa Hazina ili kuhakikisha kwamba yale ambayo hayazalishi kwa kiwango kinachostahili huenda yakafutwa ama yakaunganishwa na mashirika mengine ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi katika shughuli za uzalishaji.
“Kuna taasisi ambazo ni muhimu sana lakini zimekuwa zikifanya vibaya sana hizo tutaziweka kwenye angalizo maalum na tunazipa jicho la karibu sana kuhakikisha kwamba zinabadilika, kuna taasisi zingine ambazo hazifanyi vizuri na pia zimepitwa na wakati, ni dhahiri kuwa hizi tunaenda kuzifuta, na zile ambazo bado zinatakiwa tutaendea kuziboresha kwasaidia wale viongozi waliopo wasiposaidika tutatafuta wengine kwasababu wakati mwingine taasisi huwa hazina shida, shida ni uongozi.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege amesema kuwa benki hiyo itahakikisha inatimiza malengo yake yake ya msingi ya kuanzishwa kwake ambayo ni kuongeza tija na kusimamia shughuli za kilimo kwa kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija kwa mkulima na taifa kwa ujumla.
“Benki hii wakati inaanzishwa ilikuwa na malengo ya kusimamia usalama wa chakula nchini, pili kusaidia kufanya mageuzi ya kutoka kwa wakulima wa nchi yetu kutoka katika kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kilimo cha kibiashara, hivyo benki ya kilimo tumeelekezwa kutoa mitaji kwa wakulima, ili kuhakikisha kwamba kilimo chetu kinabadilika kutoka kuuza malighafi na kwenda kuuza bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini.” Amefafanua Mkurugenzi huyo.
Bwana Nyabundege amesema kuwa kwa sasa wana mpango wa kupanua wigo wa utoaji wa huduma hususani kupitia ofisi za kanda ambapo mpaka sasa benki hiyo ina ofisi sita za kanda, ambazo ni Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Mashariki na Kanda ya Kusini.
“Benki iko mbioni kufungua rasmi ofisi mbili mpya, za kanda ambazo ni Kanda ya Kaskazini itayohudumia, mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Tanga, pia tuna mpango wa kufungua ofisi ya Kanda ya Zanzibar, na ofisi zote hizi zinatarajiwa kuwa tayari ndani ya mwaka huu.” Amefafanua Nyabundege.
Mkutano huo umeandaliwa na Ofisi ya Msajili ya hazina na Benki ya maendeleo ya Kilimo nchini wenye malengo yakiwa ni kuelezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na benki hiyo kwa wahariri na waandishi wa vyombo vya habari.








