Home Kitaifa HELSB YAZINDUA KAMPENI YA “FICHUA KUWA HERO WA MADOGO”

HELSB YAZINDUA KAMPENI YA “FICHUA KUWA HERO WA MADOGO”

Na Magrethy Katengu – Dar es Salaam

Bodi ya Mikopo Tanzania (HELSB) imezindua kampeni inayoitwa “Fichua Kuwa Hero wa Madogo“, ambapo imeomba wananchi kuwafichua wanufaika wa mikopo ambao wana vipato na kazi, lakini hawajarejesha fedha hizo, ili kusaidia wanavyuo wengine kunufaika.

Ombi hilo limetolewa leo Juni 28, 2024 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa HELSB, Dkt. Bill Kiwia, wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ya kizalendo itakayodumu miezi miwili. Katika kampeni hii, kila mtu anayemfahamu mnufaika wa mikopo hiyo anaye kipato au ameajiriwa na taasisi au kampuni, atahimizwa kutoa taarifa kuhusu huyo mnufaika kwa kutuma majina yake matatu, chuo alikosoma, na mahali alipo ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Daima tunafahamu kuwa wadaiwa wetu wengi wameajiriwa na taasisi binafsi au makampuni, na wengine wamejiajiri na wanapata vipato lakini hawataki kurejesha mikopo waliyopewa wakiwa vyuoni. Kampeni hii inalenga kuomba ushirikiano wa wananchi wote ili tuweze kusaidiana kuwafichua, ili wengine nao waweze kunufaika,” alisema Dkt. Kiwia.

Aidha, alieleza kuwa hali ya urejeshwaji mikopo kwa sasa ni nzuri ambapo wanakusanya bilioni 15 kwa mwezi, ambayo ni sawa na 70% zaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita. Kampeni hii inalenga kupunguza malalamiko ya baadhi ya wanavyuo kuhusu ukosefu wa fedha za kutosha kwa maisha yao.

Mpaka sasa, HELSB inadai jumla ya trilioni 2.1 na imekusanya trilioni 1.3, hivyo kupitia kampeni hii wanatarajia kukusanya bilioni 200 kwa ajili ya wanafunzi elfu 50.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote, ikiwa ni pamoja na mama, kaka, dada na wanafunzi waliowahi kunufaika na mikopo ya elimu ya juu, kuwa wazalendo kwa kutoa taarifa za wale ambao hawajarejesha kwa kutuma ujumbe kwa simu kwenye namba 0739665533 au kupiga simu kwenye 0736665533 wakiambatanisha majina matatu, vyuo walivyosoma, na mahali walipo sasa, ili kusaidia wengine kunufaika. Hii ni kwa kuwa kuna wanafunzi ambao hawana wazazi wote, na wengi wao familia zao zina vipato duni hivyo wanashindwa kumudu karo ya vyuo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Urejeshaji na Urekebishaji Mikopo, CPA George Mziray, amesema kwamba dirisha la mikopo limefunguliwa kwa wanafunzi wote waliohitimu kidato cha sita na wanahitaji kwenda vyuoni, na wanaweza kuomba mikopo kupitia mtandao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!