NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,amewataka Viongozi na Watendaji wa CCM kuanzia ngazi za Mashina hadi Mikoa Kichama kuratibu na kufuatilia changamoto zinazowakabili Wananchi na kuziwasilisha katika ngazi za juu za kiutendaji zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu.
Hayo ameyasema katika muendelezo wa ziara yake na Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC CCM Taifa Zanzibar ya kuimarisha uhai wa Chama, katika Mkoa wa Magharib Wilaya ya Mfenesini Kichama wakati akizungumza na wanachama katika Tawi la CCM Mwanyanya Unguja.
Dkt.Dimwa, alisema kipaumbele cha CCM ni kuhakikisha kila mwananchi anaishi maisha bora na yenye hadhi yanayoendana na kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Chama Cha Mapinduzi kinaamini kuwa Wanachama na Wapiga kura wapo katika ngazi za Matawi na Mashina yetu hivyo dhamira yetu ni kuwatumikia kwa uadilifu kwani mlituamini na kutupa ridhaa kubwa ya kuongoza nchi.
Kila mtu anaona kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi, kila sehemu ya Zanzibar kuna Hospitali za kisasa zenye vifaa tiba vyote, Skuli za ghorofa, barabara za lami, uwekezaji wananchi kiuchumi na maji safi na Salama yote haya yametekelezwa mijini na vijijini.“,alisema Dkt.Dimwa.
Aidha aliwataka Wanachama hao kuendelea kuhamasisha Wananchi wengine kujiunga na CCM ili kupata idadi kubwa ya wapiga kura wa uhakika.
Akizungumza na wanachama wa CCM katika Wadi ya Bububu shina namba 12, aliwataka wafanye kazi ya kuimarisha uhai wa Chama katika ngazi hiyo kwa kulipa ada kwa wakati.
Kupitia ziara hiyo aliwapongeza Viongozi wa majimbo yote ya Wilaya ya Mfenesini Kichama wakiwemo Wabunge,Wawakilishi na madiwa kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Pamoja na hayo aliwasisitiza Wanachama na Wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la Wapiga kura kwa awamu ya pili ili kupata takwimu sahihi.
Katika ziara hiyo Naibu Dkt.Dimwa, ameambatana na Wakuu wa Idara za CCM Zanzibar pamoja na Manaibu Makatibu wakuu wa Jumuiya zote.