Na Mwandishi Wetu.
Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imeendelea kuonyesha nafasi yake muhimu katika kukuza teknolojia na ubunifu nchini, kwa kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya 22 ya Siku ya Wahandisi Kitaifa katika Viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam. Ushiriki wa DIT umelenga kuonyesha uwezo wa wahandisi wake na wanafunzi katika kutengeneza bidhaa zinazobadilisha maisha ya jamii na kukuza ajira.
Moja ya kivutio kikuu kilichowashangaza na kuwavutia wageni waliotembelea banda la DIT ni bidhaa bora za ngozi zinazotengenezwa na wanafunzi na wahadhiri, zikiwemo viatu vya ngozi, mipira ya miguu, mikanda na bidhaa nyingine zenye ubora wa kimataifa.
Mhadhiri wa DIT Kampasi ya Mwanza, Eng. Sharifu Mwangi, aliwahimiza wazazi na jamii kuwatia moyo vijana kujiunga na DIT, hususan katika fani ya teknolojia ya ngozi.
“Ujuzi wa kutengeneza bidhaa za ngozi si tu kwamba unajenga msingi wa ajira binafsi, bali pia humfanya kijana kuwa mbunifu na mjasiriamali mwenye uwezo wa kufungua milango ya mafanikio ndani na nje ya nchi,” alisema Eng. Mwangi.
Aidha, mdau wa sekta ya ngozi kutoka Tanzania Leather Association, Bw. Abdallah Hussein, amepongeza jitihada za DIT na kusisitiza kuwa bidhaa za ngozi zinazozalishwa na taasisi hiyo zina nafasi kubwa ya kushindana kwenye soko la Afrika Mashariki na kwingineko.
Bunifu nyingine iliyowavutia Wahandisi wengi na watembeleaji wa Maadhimisho hayo ni vifaa maalum vya elimu ya vitendo vinavyojulikana kama Train Kits, vilivyobuniwa na Wanafunzi wa DIT na kutengenezwa hapa Tanzania kwa kutumia rasilimali za ndani.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Wahandisi Kitaifa Hosea Kimaro, mwanafunzi wa DIT na Mkurugenzi Mtendaji wa Honic Company Limited, amesema kuwa Train Kits zimetengenezwa kusaidia shule na taasisi mbalimbali kutatua changamoto ya upungufu wa vifaa vya majaribio, changamoto iliyokuwa ikizuia wanafunzi kujifunza masomo ya sayansi na teknolojia kwa vitendo.
“Vifaa hivi ni nafuu na vinaweza kupatikana kwa urahisi na shule nyingi. Lengo letu ni kuziba pengo lililopo kati ya elimu ya nadharia na ile ya vitendo,” amesema Hosea.
Amesema kuwa vifaa hivi vitasaidia kuongeza ufanisi katika ufundishaji wa masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na fani nyingine zinazohitaji mafunzo ya vitendo.
Aidha, mradi huo unalingana na sera ya sasa ya elimu nchini, inayolenga kutoa elimu ya amali, ambapo wanafunzi wanapata ujuzi unaoweza kutumika moja kwa moja kazini au katika maisha halisi.
Hosea ameongeza kuwa kupitia Honic Train Kits, kampuni yake inachangia moja kwa moja katika utekelezaji wa dira ya elimu ya Tanzania, ikihakikisha kuwa wanafunzi wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
Bunifu nyingine zilizowavutia watu wengi , ni Bajaji na Baiskeli za umeme pamoja na teknolojia ya kubadilisha mfumo wa magari na bajaji kutoka kutumia mafuta kwenda kwenye matumizi ya umeme , Teknolojia ya Utengenezaji wa Vipuri vya Bajaji , Mashine ya kukausha mboga na Bunifu nyinginezo.
Akizungumza na Mwandishi wetu , Mhadhiri kutoka DIT Dkt. Triphonia Ngailo alisisitiza umuhimu wa maadhimisho haya akieleza kwamba “Siku ya Wahandisi ni jukwaa muhimu linalowawezesha wahandisi kutoka sekta mbalimbali kubadilishana mawazo na uzoefu, na DIT ni chachu ya maendeleo kwa taifa kupitia mafunzo yake ya vitendo na teknolojia bunifu, aidha amewasisitiza wanawake kusoma masomo ya sayansi ili kuwa na idadi kubwa ya Wahandisi wanawake .