
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, ametembelea banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma na kupongeza mchango wa benki hiyo katika kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Mhe. Chande amesema TADB imeendelea kutekeleza jukumu lake kwa ufanisi kupitia utoaji wa huduma za kifedha zinazowawezesha wakulima, wafugaji na wadau wengine wa mnyororo wa thamani wa kilimo kuongeza uzalishaji na tija.
Amesema jitihada hizo zina mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wananchi na kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta ya kilimo.
Akiwa katika banda hilo, Naibu Waziri amepata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na TADB, ikiwemo mikopo kwa wakulima na wawekezaji wa sekta ya kilimo, pamoja na programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha vijana, wanawake na wajasiriamali wa kilimo.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono taasisi zinazowezesha maendeleo ya kilimo kwa kuwa sekta hiyo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi na chanzo kikuu cha ajira kwa Watanzania wengi.
Maonesho ya Nanenane yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za umma na binafsi kuonesha teknolojia, huduma na fursa mbalimbali zinazochochea maendeleo ya sekta ya kilimo, huku TADB ikiwa miongoni mwa taasisi zinazotoa elimu na huduma za kifedha kwa wadau wa sekta hiyo.









