Home Kitaifa BRELA, WADAU WAPITIA RASIMU YA KANUNI ZA WAMILIKI MANUFAA WA MAJINA YA...

BRELA, WADAU WAPITIA RASIMU YA KANUNI ZA WAMILIKI MANUFAA WA MAJINA YA BIASHARA

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imekutana na Mawakili, Wanasheria, Wahasibu na Washauri wa Biashara, ili kupitia rasimu ya kanuni za Wamiliki Manufaa wa Majina ya Biashara yanayomilikiwa na Wabia.

Akifungua warsha hiyo leo tarehe 01 Disemba, 2022 katika ukumbi wa Chuo cha Utalii, Jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amesema, lengo kuu ni kujadili rasimu ya Kanuni za Wamiliki Manufaa wa Majina ya Biashara yanayomilikiwa kwa ubia.

Hatua hiyo inafuatia marekebisho ya Sheria ya Majina ya Biashara, Sura 213, yaliyofanyika kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 (Finance Act , 2022) ambapo,pamoja na mambo mengine, wamiliki wa Majina ya Biashara wenye ubia (partnership) wanatakiwa kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa (Beneficial Owners) kwa Msajili wa Majina ya Biashara.

Bw. Nyaisa amesema marekebisho hayo ya sheria yalifanywa kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa wa Majina ya Biashara kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa sheria mbalimbali zikiwemo Sheria za Kodi , Uwezeshaji Kiuchumi Wananchi, pamoja na Sheria dhidi ya ufadhili wa ugaidi.

Pia amesema BRELA ikishirikiana na wataalamu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, imeandaa rasimu ya kanuni chini ya sheria ya Majina ya Biashara, Sura 213 zitakazowezesha uwasilishaji, utunzaji na utoaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa, ikiwa ni pamoja na kuandaa Daftari la Wamiliki Manufaa.

Bw. Nyaisa amesema, Wakala imeona ni vyema kuwashirikisha wadau mbalimbali kujadili na kukusanya maoni yao, ili kuboresha rasimu ya kanuni zilizoandaliwa na kuweka utaratibu madhubuti, utakaowezesha upatikanaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa wa Majina ya Biashara, pamoja na utoaji wa taarifa hizo kwa vyombo vya upelelezi vilivyoainishwa kwenye Sheria, pale zinapohitajika.

ā€œ Ni matarajio yangu kuwa, katika warsha hii tutabaini na kuepuka muingiliano kanuni zinazoandaliwa na sheria nyingine, ili kanuni hizi zitumike ipasavyo bila kuathiri taasisi nyingine, pamoja na kujadili mapungufu yaliyomo kwenye rasimu ya kanuni hizi na namna sahihi ya kutatua au kuondoa mapungufu na kupata kanuni zitakazotekelezeka na kuleta tija katika kuchochea biashara na uwekezaji, ili kukuza uchumi wa nchiā€œ, amefafanua Bw. Nyaisa.

Aidha, Bw. Nyaisa amewashukuru wadau kwa ushirikiano mzuri na kuahidi kuboresha huduma kwa njia ya mtandao, kushughulikia changamoto mbalimbali, pamoja na kupokea maoni yatakayowezesha kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!