Home Kitaifa BIDHAA ZA NGOZI ZA DIT ZATIKISA MAADHIMISHO YA 22 YA SIKU YA...

BIDHAA ZA NGOZI ZA DIT ZATIKISA MAADHIMISHO YA 22 YA SIKU YA WAHANDISI KITAIFA DAR ES SALAAM.

Na Mwandishi Wetu.

Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) kupitia kampasi yake ya Mwanza imeshiriki Maadhimisho ya 22 ya Siku ya Wahandisi Kitaifa yanayoendelea mwaka huu kwenye Viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam,na kuendelea kuonyesha ubunifu na mchango mkubwa katika maendeleo ya teknolojia ya uchakataji na usindikaji wa bidhaa za ngozi nchini. 

Moja ya kivutio kikuu kilichowashangaza na kuwavutia wageni waliotembelea banda la DIT ni bidhaa bora za ngozi zinazotengenezwa na wanafunzi na wahadhiri, zikiwemo viatu vya ngozi, mipira ya miguu, mikanda na bidhaa nyingine zenye ubora wa kimataifa.

Mhadhiri wa DIT Kampasi ya Mwanza, Eng. Sharifu Mwangi, aliwahimiza wazazi na jamii kuwatia moyo vijana kujiunga na DIT, hususan katika fani ya teknolojia ya ngozi.

 “Ujuzi wa kutengeneza bidhaa za ngozi si tu kwamba unajenga msingi wa ajira binafsi, bali pia humfanya kijana kuwa mbunifu na mjasiriamali mwenye uwezo wa kufungua milango ya mafanikio ndani na nje ya nchi,” alisema Eng. Mwangi.

Kwa upande wake, Eng. Manyama Mazubu Makankila, Mhadhiri Msaidizi wa Mitambo DIT Mwanza, alisisitiza umuhimu wa maadhimisho haya akieleza kwamba “Siku ya Wahandisi ni jukwaa muhimu linalowawezesha wahandisi kutoka sekta mbalimbali kubadilishana mawazo na uzoefu, na DIT ni chachu ya maendeleo kwa taifa kupitia mafunzo yake ya vitendo na teknolojia bunifu.”

Aidha, mdau wa sekta ya ngozi kutoka Tanzania Leather Association, Bw. Abdallah Hussein, amepongeza jitihada za DIT na kusisitiza kuwa bidhaa za ngozi zinazozalishwa na taasisi hiyo zina nafasi kubwa ya kushindana kwenye soko la Afrika Mashariki na kwingineko.

DIT kupitia Kampasi ya Mwanza imeonesha wazi kuwa teknolojia si lazima iwe mashine kubwa pekee, bali hata ubunifu katika bidhaa za kila siku kama viatu, mikoba, walleti na mikanda unaweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira na maendeleo ya taifa. 

DIT imeendelea kuthibitisha kuwa ni taasisi ya mfano inayowaandaa vijana kielimu na kwa vitendo, ikiwapa ujuzi wa kuwa wabunifu, wajasiriamali na wahandisi wa kesho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!