Home Kitaifa AWESO AJIRIDHISHA UTOSHEVU WA MAJI BWAWA LA MTERA.

AWESO AJIRIDHISHA UTOSHEVU WA MAJI BWAWA LA MTERA.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) mapema leo amefika katika Bwawa la Maji la Mtera na kujiridhisha na kiwango cha maji kilichopo katika Bwawa hilo.

Mhe. Aweso amefanya ziara hiyo kuona uhalisia na utoshelevu wa maji katika bwawa hilo kutumika kama chanzo cha ziada ya huduma ya maji katika jiji la Dodoma akiwa na wataalamu wa sekta mtambuka.

Amesema Jiji la Dodoma linaweza kuwa na chanzo cha maji zaidi ya kimoja, na maji yanayoweza kuchukuliwa katika bwawa hilo ni zaidi ya lita milioni 133, ambayo yatahudumia wakazi wa Dodoma ambapo Bwawa la Mtera lina uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo milioni 3,700 likijaa.

“ Maji isiwe sababu ya kukwamisha maendeleo ya wananchi wa Dodoma na nchi yetu” Waziri Aweso amesema na kuongeza kuwa atafanya kikao na Waziri wa Nishati ili kuona namna bora ya kuwasaidia wakazi wa Dodoma katika mpango huo wa muda mfupi wa kutumia Bwawa hilo kama chanzo cha maji.

Amefafanua kuwa mpango wa muda mrefu ni kutumia maji kutoka ziwa Victoria ili yatumike katika shughuli mbalimbali za kiuchumi jijini Dodoma, kwa sababu hivi sasa mahitaji ya maji ni lita milioni 133, na yanayozalishwa ni lita milioni 67, hivyo Dodoma ina upungufu wa lita milioni 66 na kama viongozi wanalojukumu la kufanyia kazi.

Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Rufiji Bw. Florence Mahay amesema wao kama bonde wanasimamia rasilimali za maji ipasavyo, na maji yatakayochukuliwa katika Bwawa la Mtera hayatakuwa na madhara katika kazi ya kuzalisha umeme kwa sababu yatakuwa asilimia moja ya maji yanayotumika katika kazi hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph akiongea katika ziara hiyo amesema ongezeko la watu limekuza mahitaji ya huduma ya maji, na mradi wa kuongeza maji kutoka Bwawa la Mtera utafikisha jumla ya lita milioni 201 ambazo zitaweza kutumika kwa miaka 13 ijayo jijini Dodoma.

Pamoja na hayo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri amepongeza hatua ya kuwa na vyanzo zaidi ya kimoja kwa huduma ya maji, na kusisitiza maji ni muhimu katika maeneo mtambuka kuanzia makazi hadi katika miradi mikubwa, viwanda na mifugo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!