Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma mjini, Vedastus Mathayo amekutana na VIJANA 300 wa jimbo la Musoma mjini aliowawezesha miradi ya ufugaji kuku.
Vijana waliowezeshwa kwa awamu ya kwanza ni kutoka Kata 10 kati ya 16 zilizopo kwenye jimbo la Musoma mjini.
Kila vijana 30 kwenye Kata hizo wamewezeshwa vifaranga 100,chakula cha kuku na fedha ya dawa ili kuweza kukuza vifaranga.
Akizungumza na vijana hao nyumbani kwake Mathayo amesema analidhishwa na namna alivyopata taarifa ya kuendelea vizuri.
Amesema miradi hiyo ya ufugaji wa kuku ikitunzwa vizuri itawainua kiuchumi na kuwafanya pochi zao kujaa.

Mathayo amesema.miradi hiyo ni mizuri na imewainua wengi na kuwataka vijana hao kuitunza na kuifanya kuwa endelevu.
“Niwapongeze vijana.nimepata taarifa miradi yaufugaji kuku inaendelea vizuri ikiwa ni pamoja kukua kwa vifaranga”
“Muendelee kuitunza ili vifaranga vikue baadae mtaona manufaa yake pale mtakapoanza kuwauza kuku wenu na kupata fedha”, amesema Mathayo.
Aidha mbunge huyo amewataka vijana kwenye Kata 6 zilizosalia kuendelea kuunda vikundi vya vijana 30 na kuandaa mabanda ili waweze kuwezeshwa kwa kipindi kinachofuata.
Amesema lengo ni kuwafikia vijana kwenye Kata zote 16 na kuwawezesha vifaranga kwaajili ya ufugaji wa kuku.
Kwa upande wa vijana hao wameendelea kumshukuru mbunge Mathayo kwa kuwajali na kuahidi hawawezi kumuangusha.









