Na Theophilida Felician Kagera.
Baadhi ya vijana kutoka Kijiji cha Maruku kata Maruku Halmashauri ya Bukoba Mkoani Kagera wamejiunga pamoja na kukitembelea kituo cha kulelea watoto yatima Ntoma kilichopo kata ya Maruku Halmashauri ya Bukoba.
Vijana hao wakiwa 15 wameeleza kuwa wamewiwa na kujichanga changa vitu kadhaa walivyovipeleka kituoni hapo.

Mwenyekiti wa vijana hao Frank Kachuma akitoa taarifa baada ya kukabidhi vitu walivyowapelekea watoto amesema kuwa kilicho wasukuma kufika kitoni hapo ni kuguswa na hali ya maisha ya watoto wanaoishi katika kituo hicho hivyo ikawabidi kujichanga changa hatimaye kuwatembelea watoto hao.
Mwenyekiti amevitaja vitu walivyo fanikiwa kuvitoa kwa watoto ni pamoja na sukari, sabuni, ndizi na maziwa.
Vijana hao ambao wanajishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo udereva wa pikipiki, (boda boda) fundi selemala na migahawa wamefafanua kuwa wamejipanga kuyafanya mambo makubwa yakuifikia jamii ya Maruku kupitia makundi tofauti tofauti kama kilivyo kituo hicho cha Ntoma.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Maruku Ladislaus Aloyce Kalugendo akiambatana na vijana hao amewapongeza na kuwashukuru sana vijana hao kwa namna walivyoungana na kutekeleza jambo hilo la kuvuna baraka kwa watoto hao ambapo amewasihi kuendelea kufanya mengi zaidi kwani kujitoa siku zote ni moyo.
Ametoa wito kwa vijana wengine na jamii ya Maruku kuiga mfano wa vijana hao ambao wamejitoa kwa chochote na kukifikisha kwa watoto yatima.
Peninnah K. Kaimukilwa kiongozi wa kituo hicho pia amewapongeza na kuwashukuru kwa dhati kwani siyo kawaida ya vijana kuwiwa na kufanya jambo muhimu la kijamii kama hilo la kujitoa kwa namna yoyote ile na kuwatolea sadaka watoto.
Amesema kuwa kituo hicho kilianzishwa mnamo kwama 1952 kina wafanyakazi 17 uwezo wake ni kulea watoto 30 ila kwa sasa wapo watoto 37 idadi ambayo tayari ni kubwa kuliko uwezo wakituo.
Ameongeza kwamba licha ya wadau kujitoa mara kadhaa bado kuna changamoto za uhaba wa fedha zakutosha katika kusaidia kukidhi mahitaji ya kuwalea watoto.
Kiongozi Peninnah vijana hao amewatembeza ndani ya vyumba mbalimbali wanamoishi watoto huku akiwaomba na watu wengine kuguswa na kukifikia kituo hicho.
Hata hivyo mshauri wa vijana Maruku Amos Byebazo naye amewashukuru vijana wakijiji hicho na kusisitiza kuwa kujitoa siyo jambo dogo kwa mwenye nia.
Ameiasa jamii kuona umuhimu wa kufanya mambo yenye tija kwa ajili ya watoto yatima na makundi mengine yenye uhitaji kama watoto hao.










