Na Mwandishi Wetu.
SHIRIKA la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi (TPFCS) limepata cheti cha kimataifa cha mfumo wa usimamizi wa ubora cha ISO 9001:2015, hatua inayolenga kuimarisha mifumo ya kiutendaji, kuongeza ufanisi na kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi cheti hicho, Mkurugenzi wa Uandaaji Viwango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Candida Shirima, amesema kupata cheti hicho ni hatua muhimu katika kuimarisha utendaji wa taasisi kwa kuzingatia matakwa ya viwango vinavyotambulika kimataifa.
Amesema kiwango cha ISO 9001:2015 kinahusu mifumo ya usimamizi wa ubora, inayosaidia taasisi kuweka taratibu madhubuti za utendaji, kufuatilia matokeo na kufanya maboresho endelevu kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuridhisha wanufaika wa huduma.
Hata hivyo, Dkt. Shirima amesisitiza kuwa mafanikio ya kupata cheti hicho yanapaswa kuambatana na juhudi za kukidumisha kwa kuhakikisha matakwa ya kiwango hicho yanaendelea kutekelezwa katika shughuli za kila siku za taasisi.
“Kupata cheti ni hatua moja, lakini kukidumisha ni hatua nyingine. Lazima muendelee kutimiza matakwa yake, kufuatilia utendaji na kuhakikisha mifumo inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi,” amesema.
Ameitaka TPFCS kuendelea kuboresha mifumo yake ya usimamizi na kutafuta vyeti vingine vya kimataifa vitakavyosaidia kuimarisha weledi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TPFCS, Omari Issa, amesema bodi itaendelea kusimamia utekelezaji wa matakwa ya kiwango cha ISO 9001:2015 ili kuhakikisha cheti hicho kinadumishwa na kuleta matokeo chanya katika utendaji wa taasisi.
Amesema bodi hiyo pia imejipanga kuendeleza juhudi za kupata vyeti vingine vya kimataifa katika kipindi kijacho, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha mifumo ya usimamizi na kuongeza ubora wa utendaji.
“Nawahakikishia kwamba bodi itaendelea kusimamia kwa makini si cheti hiki pekee, bali pia vyeti vingine tunavyotarajia kupata katika kipindi kifupi kijacho,” amesema Issa.
Aidha, ameiomba TBS kuendelea kuhamasisha taasisi nyingine za umma na binafsi ambazo bado hazijapata ithibati kuchukua hatua zinazostahili ili ziweze kuzingatia viwango vya kimataifa na kuboresha mifumo yao ya utendaji.
Amesema kuongezeka kwa taasisi zinazotekeleza viwango hivyo kutasaidia kuimarisha uwajibikaji, kuongeza tija na kuboresha ubora wa huduma katika sekta mbalimbali.
Kwa mujibu wa TBS, matumizi ya viwango vinavyotambulika kimataifa ni miongoni mwa hatua muhimu katika kujenga mifumo imara ya usimamizi, kuimarisha weledi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, sambamba na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Kupatikana kwa cheti cha ISO 9001:2015 ni hatua muhimu kwa TPFCS katika kuimarisha mfumo wake wa usimamizi wa ubora. Hata hivyo, mafanikio ya muda mrefu yatategemea utekelezaji endelevu wa matakwa ya kiwango hicho, ufuatiliaji wa utendaji na maboresho yanayolenga kuongeza ufanisi wa taasisi.









