
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema upatikanaji wa mitaji, uwekezaji katika viwanda na uboreshaji wa mazingira ya biashara ni muhimu katika kufanikisha malengo ya DIRA 2050, inayolenga kukuza uchumi wa Tanzania kutoka takriban dola za Marekani bilioni 100 hadi dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

Akizungumza katika mkutano wa Wadau wa Mpango wa Fedha Mbadala na Ubunifu uliofanyika wakati wa kongamano la Tanzania Startup Week 2026, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Mhe. Balozi Omar amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira yatakayowezesha wawekezaji na wafanyabiashara kuwa na shauku na ujasiri wa kuwekeza mitaji, kwa kuzingatia uelewa wa watu wanaosaidiwa pamoja na sheria zinazosimamia shughuli hizo.
Ameeleza kuwa kufikia malengo ya Dira 2050 kunahitaji mabadiliko ya kiuchumi na kimuundo yatakayoongeza uzalishaji na kuimarisha sekta zenye uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi.

“Kwa sasa, kilimo kinachangia takriban asilimia 24 ya uchumi wa Tanzania, huku sekta ya viwanda ikichangia asilimia nane, hali inayoonesha umuhimu wa kuongeza mchango wa viwanda katika muundo wa uchumi” Alisema Mhe. Balozi Omar.
Kuhusu mwenendo wa uchumi, alisema uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.6 mwaka 2024 na kufikia asilimia 5.9 mwaka uliofuata, huku lengo likiwa kufikia ukuaji wa asilimia 6.3 mwaka 2026.
Alibainisha pia kuwa mfumuko wa bei umeendelea kuwa chini ya asilimia tano, sambamba na utulivu wa viwango vya ubadilishaji fedha na nakisi ya bajeti.
Katika eneo la mikopo, alisema mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 33 kwa mwaka ulioishia Agosti huku sekta ya viwanda ikiwa haijaonesha maendeleo makubwa katika kunufaika na mikopo hiyo, jambo linaloonesha umuhimu wa kuimarisha njia mbadala za upatikanaji wa mitaji, ikiwemo mitaji ya ubia (venture capital) na uwekezaji wa hisa binafsi (private equity).
Aidha, Mhe. Balozi Omar ameeleza kuwa Serikali imejizatiti kuendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia mageuzi ya sera na mifumo ya kodi, ikiwemo likizo ya kodi ya mwaka mmoja kwa biashara changa (startups) mpya na mabadiliko ya vizingiti vya kodi, hatua inayolenga kuchochea ukuaji wa biashara changa na kuongeza uwekezaji nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia malengo ya DIRA 2050.









