Home Kitaifa WANANCHI KILOMBERO WANUFAIKA NA HUDUMA YA UMEME NA ELIMU YA NISHATI SAFI...

WANANCHI KILOMBERO WANUFAIKA NA HUDUMA YA UMEME NA ELIMU YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

📍Kilombero, Morogoro

Wananchi wa Kata ya Katindiuka, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, wameendelea kunufaika na ziara ya utoaji elimu na uhamasishaji kuhusu miradi ya nishati vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Ziara hiyo imelenga kuwafikia wananchi katika maeneo yao na kuwapatia elimu kuhusu miradi ya nishati inayotekelezwa, pamoja na kuwawezesha kupata taarifa sahihi kuhusu namna ya kutumia na kunufaika na huduma zinazotokana na miradi hiyo.

Katika zoezi hilo, wananchi wa Vitongoji vya Katindiuka A, Katindiuka B na Katindiuka C wamepata huduma mbalimbali, ikiwemo usajili wa maombi ya kuunganishiwa umeme na ufafanuzi kuhusu taratibu na masharti ya kupata huduma hiyo. Huduma hizo zimetolewa kupitia Kliniki Maalum ya Huduma za Umeme, iliyoanzishwa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za umeme.

Aidha, wananchi wamepatiwa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, hususan matumizi ya majiko ya umeme, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa na kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika jamii.

Wananchi wameelezwa kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yana mchango katika kuboresha afya za familia, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza ufanisi katika shughuli za upishi.

REA imeendelea kuhimiza wananchi kutumia fursa zinazotokana na upatikanaji wa huduma ya umeme vijijini, ikiwemo kutumia umeme kama chanzo cha nishati safi ya kupikia, sambamba na kushiriki katika programu za uhamasishaji zinazolenga kuongeza uelewa kuhusu matumizi salama, bora na yenye tija ya nishati.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!