Home Kitaifa TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA PILI WA AFRIKA NA GCC PLUS...

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA PILI WA AFRIKA NA GCC PLUS KUHUSU AJIRA

Na Magrethy Katengu— Mzawa media Dar es Salaam

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano mkubwa wa pili wa Afrika na nchi za Ghuba (GCC Plus), utakaolenga kuimarisha ushirikiano katika masuala ya uhamaji wa wafanyakazi,ajira na mahitaji ya soko la ajira kati ya nchi za Afrika na Mataifa ya Kiarabu.

Mkutano huo ujulikanao Doha Dialogue-, Il utakaofanyika Oktoba 5 na 6 mwaka huu utawakutanisha wanachama wa Umoja wa Afrika(AU), nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (GCC), ambazo ni Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Qatar, Kuwait, Oman na Bahrain, pamoja na Jordan na Lebanon.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Septemba 28,2026 Jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira,na Mahusiano Deus Sangu ambapo amesema Mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kujadili na kuweka mikakati ya pamoja kuhusu uhamaji salama, wenye tija na unaozingatia haki za wafanyakazi, pamoja na kukuza fursa za ajira, hususani kwa vijana.

Amefafanua kuwa Mkutano wa kwanza wa aina hiyo ulifanyika jijini Doha, Qatar, Mei 21 na 22, mwaka 2024, ukihudhuriwa na nchi 43, zikiwemo nchi 25 za Afrika, nchi za GCC pamoja na Jordan na Lebanon, kwa pamoja zikijulikana kama GCC Plus.

“Tanzania ilishiriki katika mkutano huo wa kwanza ambao ulihusisha majadiliano yaliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika na nchi za Kiarabu katika masuala ya uhamaji wa wafanyakazi.”amesema

Ameongeza kuwa Mkutano huo ulihitimishwa kwa kupitishwa kwa Azimio la Doha(Doha Declaration),lililoweka msingi wa kuendeleza majadiliano na ushirikiano kati ya pande hizo.

Halikadhalika amesema Tanzania imepata nafasi ya kuwa nchi ya pili kuwa mwenyeji wa mkutano huo, ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili, na kwa mara ya kwanza kufanyika katika bara la Afrika.

“Moja ya maeneo muhimu yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni kuimarisha uhamaji wa wafanyakazi kati ya nchi, ikiwemo makubaliano ya uhamaji (Migration Agreements), ujuzi wa wafanyakazi, mahitaji ya soko la ajira na uanzishwaji wa mifumo ya kusaidia uhamaji salama na wenye tija” amesema

Hata hivyo amefafanua kuwa Serikali imesema imeweka mfumo wa kuhakikisha Watanzania wanaopata fursa za ajira nje ya nchi wanapata mikataba ya kazi na kulindwa dhidi ya unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na kunyanyaswa kazini na kunyang’anywa hati zao za kusafiria.

Akizungumza kuhusu fursa za ajira nje ya nchi, Waziri wa Kazi na Ajira amesema Serikali imehakikisha Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi wanapitia utaratibu rasmi, huku mikataba yao ikiwa chini ya usimamizi wa mamlaka husika za Serikali.

Amesema mikataba hiyo inalenga kuhakikisha haki za wafanyakazi zinalindwa, ikiwemo viwango vya mishahara, aina ya kazi wanayopangiwa kufanya pamoja na mazingira mengine ya ajira.

Kwa mujibu wa Waziri Serikali pia imeimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Kazi na Ajira, Wizara ya Mambo ya Nje na Balozi za Tanzania katika nchi ambazo Watanzania wanakwenda kufanya kazi.

Amesema mwajiri wa nje hatakiwi kuendelea kumuajiri Mtanzania bila taarifa na utaratibu wa kibalozi, huku balozi za Tanzania zikiwekwa katika nafasi ya kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na waajiri.

“Katika Wizara kwa sasa hakuna mfanyakazi anayefanya kazi nchini bila kupitia kwenye mfumo wa Wizara. Wote tumewapa mawasiliano, wana mawasiliano ya balozi na wana mawasiliano ya Wizara. Lengo ni kuhakikisha kama changamoto yoyote inatokea wawe tayari kutujulisha mara moja na hatua stahiki zichukuliwe,” amesema.

Amesema mfumo huo umesaidia kupunguza changamoto zilizokuwa zikiripotiwa kwa Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi, ikiwemo unyanyasaji na kunyang’anywa pasipoti.

Ameongeza kuwa kuanzia Januari hadi sasa hakuna kesi iliyowasilishwa Serikalini inayohusu unyanyasaji wa Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi, huku Serikali ikiendelea kufanya ufuatiliaji kupitia balozi zake.

Aidha, amesema Serikali imeanzisha utaratibu maalumu wa kuwaandaa vijana kabla ya kuondoka nchini, ikiwemo siku maalumu ya kuwaaga na kuwapatia maelekezo kuhusu namna ya kupata msaada endapo watakutana na changamoto wanapokuwa nje ya nchi.

Amesema viongozi wa Serikali wamekuwa wakifanya ziara katika nchi mbalimbali ambako Watanzania wanafanya kazi kwa lengo la kukutana nao, kusikiliza changamoto zao na kujadiliana na Serikali za nchi hizo namna ya kuzitatua.

Ametolea mfano ziara nchini Qatar ambako viongozi wa Serikali walikutana na Watanzania wanaofanya kazi nchini humo, akisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali katika kuhakikisha nguvu kazi ya Watanzania inalindwa.

Kwa upande wa takwimu, Waziri huyo amesema kuanzia Januari hadi sasa Watanzania 8,408 wameunganishwa na fursa za ajira nje ya nchi.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili, jumla ya Watanzania 15,715 wameunganishwa na fursa za ajira katika nchi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali imeingia makubaliano na baadhi ya nchi na taasisi za ajira, hatua inayowezesha Watanzania kupata nafasi katika kada mbalimbali, zikiwemo ualimu wa vyuo vikuu, udaktari, uhandisi na utafiti.

Amesema fursa hizo zinatarajiwa kuongezeka zaidi, akitolea mfano Qatar ambako kuna mipango ya kutoa nafasi za ajira kwa wahandisi na watafiti.

Aidha, amesema kampuni kubwa ya ujenzi nchini Qatar, Holding Power, inatarajiwa kutoa takribani nafasi 4,300 za ajira kwa Watanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!