
TAASISI ya Tanzania Pathways Initiative (TPi) imeungana na jamii ya Kawe Ukwamani jijini Dar es Salaam katika zoezi la usafi wa mazingira, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha jiji linakuwa safi na salama.
Zoezi hilo pia limelenga kuhamasisha wananchi kuchukua hatua za mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotarajiwa kutokana na hali ya El Nino.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mwenyekiti wa TPi, Makumba Mwemezi, amesema usafi wa mazingira, hususan mitaro, ni muhimu katika maandalizi ya msimu wa mvua kwa kuwa taka zinazoziba mitaro zinaweza kusababisha maji kutuama na kuongeza hatari ya mafuriko.
Amesema TPi imeamua kushiriki katika shughuli hiyo kwa lengo la kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa usafi na kuchukua hatua za mapema katika kukabiliana na changamoto za mazingira.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa TPi, Pendo Sumila, amesema taasisi hiyo inalenga kusaidia na kutoa elimu kwa jamii za mijini ambazo bado zinakabiliwa na changamoto mbalimbali za maendeleo.
Amesema TPi hutoa elimu kuhusu afya, mazingira na masuala ya maisha kwa vijana, hivyo ushiriki katika zoezi la usafi ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kuelimisha na kushirikiana na jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kawe Ukwamani, Hamis Rashidi, amesema mtaa huo umejiwekea utaratibu wa kufanya usafi kila mwisho wa mwezi, akishukuru TPI kwa kuungana na wananchi katika zoezi hilo.
Rashidi amesema ushiriki wa taasisi hiyo ni muhimu katika kipindi hiki ambacho mamlaka za hali ya hewa zimeonya kuhusu uwezekano wa mvua kubwa za El Nino.









