
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka vijana wa Kitanzania wachangamkie fursa zilizopo katika sekta ya madini ili wanufaike na utajiri wa rasilimali hizo na kujenga biashara kubwa za Kitanzania.
Amesema Serikali inalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kukua na kuwa wawekezaji wakubwa, akisisitiza kuwa rasilimali za madini zinapaswa kuwanufaisha Watanzania.
“Tunataka wachimbaji hawa wadogo nao wakue, tutengeneze mabilionea wa Kitanzania; ndiyo maana rasilimali hizi zililetwa hapa Tanzania ziwanufaishe Watanzania,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Septemba 15, 2026) wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Sapiwi, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu, katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Waziri Mkuu amesema baadhi ya watu wamekuwa wakishikilia idadi kubwa ya leseni za madini kwa miaka mingi bila kuziendeleza, huku vijana wakikosa maeneo ya kufanya shughuli za uchimbaji.
“Mtu mmoja anakuwa na leseni nyingi, ameshikilia miaka 10, vijana wanatafuta pa kuchimba… hili nimemwelekeza Waziri wa Madini afanye tathmini, aliye na leseni asiyoifanyia kazi, apewe vijana wapate pa kuchimba,” amesema.
Ametoa agizo kwa Waziri wa Madini afanye tathmini ya leseni zinazoshikiliwa kwa muda mrefu bila kuendelezwa na, pale zinapobainika kutotumika kwa mujibu wa masharti, kuchukua hatua stahiki ili maeneo hayo wapatiwe vijana wenye nia ya kufanya shughuli za uchimbaji.
Kuhusu barabara, Waziri Mkuu amemwelekeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kuhakikisha barabara ya Somanda–Nkololo–Matongo–Igegu inapandishwa hadhi kuwa ya Mkoa ili iende kuhudumiwa na TANROADS.
“Hii barabara pandisheni, iende ihudumiwe na TANROADS, ipandisheni kwenye hadhi ya mkoa ili ipate uamuzi wa mwisho lakini kabla ya hapo, madaraja lazima yajengwe, wananchi wasikwame na wakati huo huo tusiwe tunapoteza maisha ya watu kwa kusombwa na maji,” amesema.
Katika sekta ya afya, Waziri Mkuu amekemea vitendo vya kuwatoza wagonjwa wanaohitaji huduma za rufaa fedha za mafuta ya ambulance, akisisitiza kuwa magari hayo yanapaswa kuwa na mafuta na dereva wakati wote.
“Mgonjwa ameshapewa rufaa anatakiwa apelekwe hospitali ya rufaa, anatakiwa apelekwe kwa haraka. Ambulance ipo, mara zote ambulance iwe na mafuta na iwe na dereva,” amesema.
Ameagiza pia watumishi wanaobainika kuwachangisha wagonjwa fedha kwa ajili ya mafuta wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeondoa utaratibu wa kutaifisha mifugo ya wananchi na kwamba sheria nyingine zinazohusiana na mifugo, wanyamapori na hifadhi zitaendelea kufanyiwa mapitio.
Aidha, amewaagiza viongozi na watendaji kuacha tabia ya kukamata vitendea kazi vya wananchi, ikiwemo pikipiki, bajaji, baiskeli na mikokoteni, kwa makosa yanayoweza kushughulikiwa kwa kutoza faini.
Kuhusu zao la pamba, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Kilimo akutane na wadau ndani ya mwezi mmoja na kuwasilisha mapendekezo ya mfumo bora wa ununuzi wa pamba utakaowanufaisha wakulima na kuongeza uzalishaji.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew, amesema Serikali imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 10 kutekeleza miradi 22 ya maji katika Jimbo la Bariadi Vijijini, huku Shilingi bilioni 3.2 zikitengwa kwa ajili ya kukamilisha miradi mitatu.
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, amesema Serikali imepokea madai 516 ya madhara yatokanayo na wanyamapori katika mwaka wa fedha 2024/2025 hadi 2025/2026, ambapo 469 yamelipwa na yaliyobaki yanaendelea kushughulikiwa.
Pia, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo John Dugange, amesema Serikali imetenga Shilingi milioni 40 kwa ajili ya usanifu wa madaraja mawili ya Duma na Gambosi, huku barabara ya Dutwa kuelekea Hospitali ya Wilaya ikiwa tayari ina mkandarasi.









