
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) imesema ushiriki wake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) unalenga kuelimisha wananchi kuhusu maboresho ya mitaala, kuhamasisha elimu jumuishi na kusogeza karibu huduma za vitabu vya kiada na ziada kwa wananchi.
Akizungumza katika maonesho hayoleo Julai 6, 2026 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amesema taasisi hiyo imejipanga kutekeleza malengo makuu matatu kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo.
Amesema lengo la kwanza ni kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu maboresho ya mitaala yaliyofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Taasisi ya Elimu Tanzania.
Dkt. Komba amesema maboresho hayo ni ya sita kufanyika tangu Tanzania ipate uhuru, hivyo TET inaendelea kuwaeleza wananchi mabadiliko yaliyofanyika na namna yatakavyoboresha utoaji wa elimu nchini.
Amefafanua kuwa wazazi wanaelimishwa kuhusu wajibu wao katika kufanikisha utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa, huku wanafunzi wakipewa ufafanuzi wa mabadiliko yaliyofanyika katika mfumo wa elimu. Aidha, walimu wanaendelea kuhamasishwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuhakikisha mtaala huo unafikia malengo yaliyokusudiwa.
Kuhusu lengo la pili, Dkt. Komba amesema TET inaendelea kuonesha namna inavyotekeleza elimu jumuishi kwa kuhakikisha kila mtoto, ikiwemo wenye mahitaji maalumu, anapata haki ya elimu.
Amesema taasisi hiyo imeandaa vitabu vya maandishi ya Braille kwa wanafunzi wasioona pamoja na vitabu vyenye maandishi yaliyokuzwa kwa wanafunzi wenye uoni hafifu, ili kuwawezesha kujifunza katika mazingira yanayowajali sawa na wanafunzi wengine.
Vilevile, amesema TET imeandaa vifaa maalumu vinavyowawezesha watoto wasioona kujifunza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kisayansi wa Kuimarisha Stadi za KKK uliozinduliwa mapema mwaka huu na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema lengo ni kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalumu wanamudu stadi hizo muhimu kabla ya kufikia darasa la tatu.
Akizungumzia lengo la tatu, Dkt. Komba amesema TET inatumia maonesho hayo kuuza vitabu vya kiada na vya ziada sambamba na kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vitabu hivyo.
Amesema sera ya vitabu inaelekeza mwanafunzi kuwa na kitabu kimoja cha kiada na vitabu vingi vya ziada, hivyo taasisi inaendelea kuwahamasisha wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata vitabu vinavyohitajika ili kuongeza ufanisi wa kujifunza.
Aidha, ametangaza kuwa katika kipindi cha Maonesho ya Sabasaba, TET imetoa punguzo maalumu la asilimia 10 kwa vitabu vya kiada vya mtaala ulioboreshwa na kuwakaribisha wananchi kutembelea banda la taasisi hiyo ili kujipatia vitabu na huduma mbalimbali zinazotolewa.









