
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetunukiwa Tuzo leo tarehe 5 Juni 2026, Siku ya Mazingira Duniani kutokana na mchango wake mkubwa katika kuendeleza kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, matumizi endelevu ya rasilimali za asili na uwekezaji katika teknolojia rafiki kwa mazingira.
Tuzo hiyo imekabidhiwa jijini Dodoma na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa ujumbe uliobebwa na tuzo hiyo, TADB imetambuliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mchango wake mkubwa katika kukuza kilimo endelevu na juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia uwekezaji na ufadhili wa miradi yenye kuzingatia uhifadhi wa mazingira.
Tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bi. Hawabai Abdulla. Hafla hiyo pia ilishuhudiwa na Katibu wa Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Alex Ndikile, pamoja na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Bi. Prudence Masako.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, mwakilishi wa TADB aliipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutambua juhudi za benki katika kukuza maendeleo ya kilimo endelevu.
Alisema kuwa tuzo hiyo inaendana na mkakati wa TADB wa kuimarisha uthabiti wa sekta ya kilimo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza uwekezaji unaozingatia utunzaji wa mazingira.









