
Tume ya Ushindani (FCC) imeanza maadhimisho ya Wiki ya Ushindani kuelekea kilele cha Siku ya Ushindani Duniani kitakachofanyika Desemba 5, ikiwa na lengo la kuongeza uelewa wa umma kuhusu athari za teknolojia ya Akili Mnemba (AI) katika ushindani wa masoko. Maadhimisho hayo pia yanahimiza utekelezaji wa sera na sheria za ushindani katika kukuza uchumi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, amesema chanzo cha maadhimisho hayo ni uamuzi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wa mwaka 1980 kupitia Kanuni za Kimataifa za Kudhibiti Vitendo Vinavyokandamiza Ushindani (The UN Set). Amesema FCC, chini ya Sheria ya Ushindani Na. 8 ya 2003, inaendelea kuhakikisha masoko yanabaki huru na shindani.
FCC inaendelea kudhibiti makubaliano yanayopunguza ushindani, matumizi mabaya ya nguvu ya soko na miunganiko ya kampuni. Kwa mujibu wa sheria, kampuni inayotarajia kufanya muamala wenye thamani ya Shilingi bilioni 3.5 au zaidi inapasa kuwasilisha taarifa kwa ajili ya uchambuzi wa ushindani. Hatua hii imelenga kuzuia ukiritimba unaoweza kudhuru maslahi ya watumiaji.
Kwa mwaka huu, FCC imechagua kaulimbiu “Artificial Intelligence (AI), Consumers and Competition Policy,” ikimaanisha “Akili Mnemba (AI), Walaji na Sera za Ushindani.” Bi. Ngasongwa amesema matumizi ya AI katika biashara yanaongezeka kwa kasi, hivyo kunahitajika uchambuzi mpana wa athari zake katika ushindani wa masoko.
Hata hivyo, pamoja na kutoa tija, AI imeelezwa kuleta changamoto kama algorithmic collusion, udukuzi wa taarifa, utapeli wa kidijitali na hatari za usalama wa taarifa. Amesema bila udhibiti madhubuti, changamoto hizo zinaweza kupunguza uwazi katika masoko, ingawa matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa sera za ushindani.
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho, FCC imeratibu shughuli mbalimbali kuanzia Desemba 1 hadi 5, zikiwemo elimu kupitia vyombo vya habari, semina kwa mamlaka za udhibiti na mafunzo kwa kampuni za sheria. Kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika katika Hoteli ya King Jada, Morocco Square jijini Dar es Salaam.








