Home Kimataifa NCHIMBI: TANZANIA NI SALAMA NA TULIVU

NCHIMBI: TANZANIA NI SALAMA NA TULIVU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imechukua hatua za kurejesha utengamano katika nchi na kuhakikisha wananchi wanaishi katika utawala wa sheria.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC), uliyofanyika kwa njia ya mtandao, akiwa mkoani Dodoma.

Amesema dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha mchakato wa mazungumzo ya maridhiano unafanikiwa ili kuwa na Taifa lenye amani na umoja na kuendelea kuwa mfano wa utulivu katika Afrika na Dunia kwa ujumla.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema Tanzania ni salama na tulivu na ipo tayari kuendelea kupokea wageni kutoka duniani kote kwa manufaa ya nchi zote.

Aidha, Makamu wa Rais, amewashukuru viongozi wa SADC walioshiriki uapisho wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wote waliotoa pongezi za dhati. Amesema jitihada zote zitatumika kuhakikisha Tanzania inapata maendeleo na amani kuendelezwa.

Mkutano huo umempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi aliyoupata na uchaguzi wenye mafanikio.

Mkutano huo ulilenga kujadili kujiondoa kwa nchi ya Madagascar kama nchi Mwenyekiti wa SADC, ambapo nchi ya Afrika Kusini imependekezwa kuwa Mwenyekiti kwa kipindi cha mpito mpaka kufikia mwezi Agosti 2026.

Mkutano huo umekubaliana kuendelea kutumia kauli mbiu ya Mkutano wa 45 wa SADC uliyofanyika nchini Madagascar ambayo ni “Kuimarisha Viwanda, Mapinduzi ya Kilimo, Mabadiliko ya Nishati kwa SADC yenye Uhimilivu”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!