Home Kitaifa HAYA NI MAPINDUZI YA MALIPO KIDIGITALI NCHINI , MIXX, TCCIA NA YAS...

HAYA NI MAPINDUZI YA MALIPO KIDIGITALI NCHINI , MIXX, TCCIA NA YAS BUSINESS WAUNGANA KUHARAKISHA

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam – 26.10.2025. Kampuni ya huduma za kifedha kwa njia ya simu, Mixx imeingia makubaliano ya ushirikiano na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) pamoja na Yas Business kwa lengo la kuimarisha malipo ya kisasa na kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini.

Hatua hii inalenga kuunganisha wafanyabiashara, wakulima, wanawake na vijana katika uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi.

Akizungumza wakati hafla ya utiaji saini jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Angelica Pesha, alisema makubaliano hayo yatasaidia kuchochea ajenda ya taifa ya uchumi wa viwanda na kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

“Kupitia huduma zetu za Mixx na ushirikiano na Yas Business, wanachama wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) watawezeshwa kupata suluhisho za malipo kidijitali, mawasiliano ya kisasa na elimu ya kifedha. Ushirikiano huu hautabaki kwenye makaratasi bali utatafsirika kwenye miradi kwa vitendo na mafanikio kwa kumgusa kila mwanachama wa TCCIA na wananchi kwa ujumla,” alisema Pesha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Bw. Oscar Kissanga, alieleza kuwa ushirikiano huu mpya unakuja wakati muafaka ambapo wafanyabiashara pamoja na wakulima wadogo wanakumbana na changamoto mbalimbali, hususan upatikanaji wa mitaji, taarifa sahihi za masoko na huduma za kisasa za kifedha.

“Sekta binafsi pamoja na wabunifu wa teknolojia kama Mixx na Yas Business ni wadau muhimu katika safari ya kuelekea kwenye uchumi wa kipato cha kati na hatimaye kipato cha juu. Ushirikiano huu unalenga kuwafungulia wanachama wetu milango ya huduma bora za kifedha na mawasiliano, hivyo kuwawezesha kushindana kwa ufanisi si tu katika soko la ndani, bali pia katika masoko ya kikanda na ya kimataifa,” alisema Bw. Kissanga.

Makubaliano hayo yamejikita katika maeneo matatu muhimu yenye lengo la kuleta mageuzi katika mazingira ya biashara nchini, ambayo ni:

1. Kuimarisha mifumo ya malipo ya kidijitali kwa wanachama wa TCCIA kupitia huduma bunifu za kampuni ya Mixx, ili kuongeza ufanisi, uwazi na usalama wa miamala ya kifedha.

2. Kutoa huduma za kisasa za intaneti na mawasiliano kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) kupitia kampuni ya Yas Business, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji na upatikanaji wa taarifa kwa wakati.

3. Kuwekeza katika elimu ya kifedha na ujuzi wa kidijitali kwa vijana na wanawake, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia.

Kupitia ushirikiano huu, Taasisi hizi zinatarajia kuchochea kasi ya ukuaji wa biashara zenye ushindani, kupanua wigo wa ujumuishi wa kifedha na kuweka msingi imara wa uchumi jumuishi, endelevu na wenye mnepo kwa Tanzania ya sasa na ya baadaye.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!