Na Mwandishi Wetu.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amezindua maadhimisho ya miaka 50 ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kuliagiza shirika hilo kutumia maadhimisho hayo kama fursa ya kutangaza huduma zao.
Uzinduzi huo umefanyika Septemba 18,2025 katika ofisi za TBS zilizopo Ubungo Jijini Dar es Salaam ambapo Dkt. Abdallah amesema shirika hilo linafanya kazi kubwa ya kuhakikisha viwango vya ubora wa bidhaa unafikiwa.
Amesema kaulimbiu ya maadhimisho hayo yanayotarajia kuhitimishwa desemba mwaka huu, yana kaulimbiu ya “Uhamasishaji Ubora na Usalama kwa Maisha Bora” ambayo itasaidia kuendelea kujenga uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa uzingatiwaji wa viwango vya ubora na uimarishwaji wa bidhaa na huduma za viwango.
Amesema katika kipindi cha miaka 50, TBS imepiga hatua kubwa ikiwe kupanua wigo wa utoaji huduma na kuzisogeza kwa wananchi pamoja na kuboresha mifumo ya kielektroniki.
“Katika kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, TBS imejenga heshima kubwa kimataifa kutokana na utekelezaji mahiri wa majukumu yake kwa kupata tuzo mbalimbali ikiwepo ya Mdhibiti Bora Barani Afrika na kupata daraja la juu la Shirika la Afya Duniani (WHO), kuwa wa kwanza SADC kupata Ithibati ya Kimataifa ya uthibitishaji ubora, na ilifanikiwa kupata Ithibati ya kimataifa ya mfumo wa usimamizi wa chakula” amesema Dkt. Abdallah.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt. Ashura Katunzi amesema maadhimisho hayo yatakuwa na mafanikio makubwa ikiwepo viwango vya Marathon na viwango vya business forum, na kilele cha maadhimisho hayo ambayo yatawakutanisha wadau zaidi ya mia tano wa masuala ya ubora wa viwango, viwanda na biashara kutoka ndani na nje ya nchi, uzinduzi wa kitabu cha historia ya TBS na maonesho ya biashara.