Na Shomari Binda-Serengeti
JESHI la polisi mkoani Mara kupitia kitengo cha polisi jamii kimejikita kutoa elimu kwa wananchi ikiwemo utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu.
Polisi Kata waliopo kwenye Kata mbalimbali mkoani Mara wamekuwa wakikutana na wananchi na kuwapa elimu hiyo ambayo imeonekana kuzaa matunda.
Wilayani Seeengeti polisi kata wa kata ya Mosongo Mkaguzi msaidizi Nelson Babyato amefanya kikao na wanakijiji wa Kijiji cha Kenokwe kilichopo kata ya Mosongo kujadili masuala ya ulinzi na usalama pamoja na kutoa elimu dhidi ya madhara ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto.
Katika kikao hicho Mkaguzi huyo amekemea baadhi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto unaofanywa na baadhi ya watu kwa wenza wao pamoja na watoto kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Amewaomba wanakijiji hao kuhakikisha wanaendelea kuwa karibu na jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu sambamba na kuendeleza vikundi vya ulinzi shirikishi kwa manufaa yao na mali zao.
“Ndugu zangu tumekutans hapa kupeana elimu na kuwashirikisha ili kwa pamoja tuweze kukomesha uhalifu na wahalifu”
“Jeshi la polisi lipo karibu na wananchi kupitia polisi jamii na kama tutaendelea kushirikiana kwa pamoja tutakomesha uhalifu na wahalifu” amesema
Aidha wananchi hao wametakiwa kuacha kujichukulia sheria mkononi bali watoe taarifa za wahalifu na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Naye diwani wa Kata ya Mosongo Samson Francis Mlimi amelipongeza jeshi la polisi mkoani Mara hasa kitengo cha Polisi Jamii kwa jitihada wanazofanya kwa kutoa elimu kwa jamii inayopelekea vitendo vya kihalifu kupungua kwa kasi.









