Na Scolastica Msewa, DAR ES SALAAM
Wajasiriamali wametakiwa kutumia vizuri maonyesho mbalimbali yanayoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kutangaza bidhaa mbalimbali wanazozalisha ili wapate masoko na kujipatia kipato.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam Edward Mpogolo wakati alipofanya ziara ya kutembelea mabanda ya biashara za wajasiriamali katika viwanja vya Mlimani city katika maonyesho ya kwanza ya Wakala wa Usajili wa biashara na Leseni BRELA na Wadau wake ili kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazofanywa na wajasiriamali nchini na namna wanavyohudumiwa na BRELA.
Amesema wajasiriamali hao waonyeshe bidhaa nzuri zitakazo watangaza zaidi kwa jamii inayofika kutembelea wazalishaji hao na huduma mbalimbali wanazotoa kwa jamii.
“Wito wangu kwa Wajasiriamali ni kwamba watumie Maonyesho haya vizuri kwa kutangaza bidhaa na huduma mbalimbali wanazozalisha badala ya kufurahia tu kuuza bidhaa zao”
“Unapoamua kuja kujitangaza maana yake umeamua kuja kujitanga kwa kuja na bidhaa zitakazo kutangaza zaidi kwa ajili ya maeneo mbalimbali ya tunakozalishia bidhaa zetu” amesema Mpogolo.
Amewashukuru wajasiriamali kwa kuitikia mwito wa BRELA katika maonyesho yao kwa kushirikisha Wadau wao mbalimbali wa uzalishaji na watoa huduma kwa kwenda kuonyesha shughuli na bidhaa zao mbalimbali wanazozalisha nchini.
Aidha pia amewataka BRELA na taasisi mbalimbali wezeshi za wajasiriamali kupitia BRELA kuendelea kutangaza bidhaa na huduma mbalimbali wanazozalishwa na wajasiriamali nchini kwani wengi wao hukopa mitaji katika mabanki na taasisi mbalimbali za fedha ili wapate faida kupitia ujasiriamali wao.

Mpogolo amesema Wajasiriamali hao wanachotaka ni mikopo ikiwa ni pamoja na ushauri wa kitaalamu kitu ambacho Wakala hao wamekuwa wakifanya kwa Wateja wao.
Hatahivyo amepongeza mabadiliko makubwa ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na Wajasiriamali nchini kwamba ni nzuri, bora na Zina viwango zaidi ambapo zinaweza kuuzwa kwenye super market na kwenye maduka makubwa nchini tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Ukiangalia kuna bidhaa za batiki ambazo ni nzuri zinaweza kuuzwa kwenye super market na maduka makubwa nchini” amesema Mpogolo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Halima Bulembo amewataka Wajasiriamali ambao bado hawajasajili biashara zao na kupata Leseni za BRELA wakasajili ili waweze kufanya biashara zao kwa kupata uhalali na kuaminiwa sokoni.
“Nitumie fursa hii kuwaombea Wajasiriamali wengine hasa wa Wilaya ya Kigamboni na maeneo mengine wafike BRELA wasajili biashara na kampuni zao”
“Wapo watu wanaona BRELA kama Polisi vile niwatoe hofu BRELA wanatoa elimu, ushauri na wanamsaidia Mjasiriamali kukua katika biashara zake BRELA wanasajili, wanamsaidia Mjasiriamali kutangaza bidhaa na huduma zao ili kuwakuza kwa namna moja ama nyingine” amesema Halima.
Naye Mteja aliyekamilisha hatua za Usajili wa BRELA na kukabidhiwa cheti Bi Salima Mfinasoka ameshukuru kwa huduma Bora na za haraka alizopewa hata kufanikisha kupata cheti chake cha Usajili wa biashara zake tofauti na alivyofikiria kabla ya kuja.
+++++++++++

 
            
