Na Neema Kandoro, Magu
BAADHI ya wadau wa maendeleo wilayani Magu Mkoani Mwanza wameelezea furaha yao kutokana na utayari wa kuchangia shughuli za maendeleo katika maeneo yao kwa kusema hatua hiyo ni muhimu katika kukidhi malengo waliyokusudia ambayo yana maslahi kwao.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Magu Wilbard Bandulla alisema jana wilayani hapo kuwa wananchi wanachangia ujenzi kuanzia hatua ya misingi mpaka kukamilisha boma na umaliziaji hufanywa kwa fedha za umma.
Alisema kuwa ari ya wananchi kushiriki kuchangia katika miradi ya maendeleo kwenye sehemu zao ni kubwa akitolea mfano ujenzi wa shule ya sekondari Igekemeja katika Kata ya Kisesa.
Bandulla aliongeza kusema kuwa vilevile ujenzi wa nyumba ya Kituo cha Afya Ihayabuyaga katika Kata ya Bukandwe na Lutale nyumba ya mwalimu.
Aliongeza kusema kuwa vilevile juhudi za wananchi zimedhihirika kwenye umaliziaji wa vyumba vya madarasa Sagini na Kandawe Sekondari.
“Tunashukuru kwa namna wananchi wetu wanavyounga mkono juhudi za serikali katika kumalizia miradi wanayoletewa katika maeneo yao mbalimbali” alisema Bandulla.
Naye Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo ambaye pia ni diwani wa Kata ya Sukuma Faustine Makingi alisema kuwa upo mwitikio mkubwa kwa jamii kuchangia kwenye miradi yao ya kimaendeleo katika sehemu zote wilayani hapo.
Alisema miradi inayotelekezwa na Mfuko wa Kunusuru Kaya Masikini Tanzania TASAF katika maeneo mengi inamwitikio mkubwa wa wananchi kuchangia kukukamlisha miradi wanayoletewa.
“Kuna sehemu tulihamasisha kuchangia kukamilisha miradi yao hivyo sisi viongozi tulitoa michango baadaye tukawauliza hizi fedha tulizochanga mnywe soda ama muuongezee kwa ajili ya mradi wenu na kura zilipigwa waliotaka fedha zielekezwe kwenye mradi walishinda” alisema Makingi.
Kijiji cha Nyigogo Kata ya Ilungu wamechangia ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi, shule mpya ya Msingi Mwamakanza.








