

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kukuza Sekta ya Utalii ikilenga kufikia watalii wa ndani na wa nje milioni nane (8) ifikapo mwaka 2030.
Ameyasema hayo alipokuwa analihutubia na kufungua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 14, Novemba, 2025, Bungeni jijini Dodoma.

“Kutokana na wingi na ubora wa vivutio vya utalii pamoja utamaduni mkubwa wa kiutamaduni Tanzania tunaweza kufikia lengo hili na tutafungamanisha vivutio vya utalii ili mtalii atumie siku nyingi zaidi akiwa nchini Tanzania.” amesisitiza Rais Samia na kusema sekta hiyo ina mchango mkubwa sana kwenye Uchumi.
Aidha, Rais samia ameahidi kuboresha vyuo vya utalii na ukarimu kwa kuongeza idadi ya watoa huduma wenye weledi katika fani zote kwenye sekta hiyo ya utalii na ukarimu.
‘Sekta hii nayo ni sehemu muhimu ya kuzalisha ajira kwa wananchi na kutuongezea akiba ya fedha za kigeni’ amesema Rais Samia.
Pia, Rais Samia amefafanua kuwa Serikali itaendeleza jitihada za uhifadhi na utunzaji wa maliasili sambamba na kupambana na ujangili.
“Hatuna budi kuongeza nguvu kukabiliana na changamoto ya wanyama waharibifu inayokabili jamii mbalimbali zinazopakana na hifadhi kote nchini’ amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema pia Serikali itaongeza askari ,vituo vya ulinzi,mbinu na vifaa vya kisasa ikwemo ndegenyuki kwa kukabiliana na janga la wanyama waharibifu.








