Home Kitaifa TUPINGE UKATILI WA JINSIA WADAU WA MICHEZO WAPEWA WITO

TUPINGE UKATILI WA JINSIA WADAU WA MICHEZO WAPEWA WITO

Na Mwandishi wetu

Naibu Waziri wa Michezo,Sanaa na Utamaduni Hamis Mwinyijuma(Mwana FA) ameziomba Timu za Mpira Nchini kuungana kuisaidia jamii katika mambo mbalimbali kukemea vikali vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji ,ulawiti ili kuwa na Taifa imara na lenye maendeleo Jumuishi.

Wito huo ameutoa Jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Thamani Women Tanzania ulikwenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto kupitia mchezo wa mpira wa miguu ambapo Club tatu za mpira wa miguu za Simba SC,Singida Fountain gate SC na Azam Sc zimeungana na Taasisi ya Thamani Women Tanzania katika kupinga ukatili.

Mwinyijuma amesema Michezo imekuwa na uwezo wa kuwaunganisha watu na jamii na ina nguvu kubwa katika miktadha yote na kuwaunganisha Kuanzia watu wa kiwango cha taaluma ya juu kabisa mpaka chini,watu wenye vipato tofauti,matabaka na dini tofauti.

“Jambo hili linapelekea mpira kuwa zaidi ya mchezo bali zana muhimu ya kuvunja vizuizi vya kijamii na kitamaduni nje ya uwanja; wachezaji kutoka nyanja mbalimbali wana jukumu la kufanya kazi pamoja kufikia lengo moja: ushindi dhidi ya timu pinzani.Mabibi na Mabwana, Leo tuna-shuhudia vilabu hivi vitatu vikiungana dhidi ya mpinzani mmoja Ukatili”.

Ameongeza kuwa Takwimu za tafiti tofauti,zinaonyesha kuwa, asilimia 40 ya wanawake wote wenye umri wa miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili, wakati asilimia 17 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia na Kati ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49, asilimia 44 wamefanyiwa ukatili wa kimwili au wa kijinsia na wenza wa karibu Nchini Tanzania.

“Kwa Kipindi kirefu sana swala la kupinga ukatili limekuwa likiongelewa na wanawake, ni wakati muafaka wa sisi vijana wa kiume,kina baba wa makamu tofauti tulijadili hili janga la kitaifa ili turithishe watoto wetu taifa lenye utulivu, amani,upendo na maendeleo. Wanawake wana mchango mkubwa sanaaa katika maendeleo ya taifa la Tanzania na maendeleo yetu wanaume kwa ujumla. Nimeona FIFA na mashirikisho tofauti ya mpira duniani yakitumia mchezo wa mpira kutetea haki za binadamu;niwapongeze sana THAMANI WOMEN TANZANIA kwa kutumia michezo kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kijinsia”.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu na mwanzilishi wa taasisi ya THAMANI Bi Nafue Nyange amesema kampeni hiyo inalenga vijana wa jinsia ya kiume kuanzia umri wa miaka 13 na wanaume wa makamu kuendelea; kwa kuwashirikisha wanamichezo kupaza sauti kupinga ukatili wa Kijinsia wanaimani wanaume watasikia kwani ndio mashabiki wakubwa wa mpira.
“Ni lazima Vijana wa kiume watambue ya kwamba katika janga hili wao ni suluhu na sio tatizo tu kwahivyo ni muhimu wajadili tatizo hili.The male youth must understand that they are part of the solution not the problem,hence it is key that they have this conversation. Ukatili sio ujanja, ni udhaifu…wanaume wanajukumu la kulinda na kuhudumia sio kupiga na kuumiza, piga mpira sio Mwanamke.

.

“Amani ya watoto wako ya sasa na baadae inaanza na amani ya mama na utulivu wa nyumbani. Na kwa sasa niseme Kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia ya PIGA MPIRA SI MWANAMKE imezinduliwa rasmi”. Amesema Nafue.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Simba Sc Imani Kajula amesema kuwa thamani ni kitu chenye faida kubwa na kinafungamanishwa na na mwanamke kwani ni mtu wa thamani kubwa kwenye jamii, “Mama wanamchango mkubwa katika mafanikio ya mtoto, mama akiwa na msongo wa mawazo ama ananyanyasika watoto pia huathiriwa pakubwa na kishindwa kutimiza ndoto zao ipasavyo”

Ameongeza ukatili wa kijinsia unapaswa kukemewa na watu wote,hivyo amewataka mashabiki wa Simba Sc kupaza sauti zao na kutokuwa miongoni mwa watu wanaofanya vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake.

Aidha Taasisi ya Thamani Women Tanzania imeomba Serikali na wadau wa michezo Nchini kuibeba kampeni hiyo yenye ujumbe usema “Piga mpira sio mwanamke” kwa kuweka kwenye mabango mbalimbali kwenye viwanja vya mpira ili kila shabiki na watazamaji wa mpira waweze kufikiwa na kwa kufanya hivyo kutasaidia kufikisha ujumbe kwa watu wengi na kwa muda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!