
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefungua kituo kipya cha huduma katika eneo la Masaki Dar es Salaam ambacho kipo chini ya mkoa kodi Kinondoni lengo likiwa ni kuendelea kusogesa huduma kwa wananchi na kurahisisha ulipaji wa kodi.
Akizindua kituo hicho Februari 17,2026 Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema kufunguliwa kwa kituo hicho kunatokana na masaki kuwa eneo la kimkakati la biashara hivyo kitawawezesha watu wote wanaostahili kulipa kodi katika eneo hilo kulipa kodi wanazostahili.

Amesema kufunguliwa kwa kituo hicho pia ni miongoni mwa mikakati ya TRA ya kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza wigo wa kodi hali ambayo inaweza kupunguza viwango vya kodi katika siku za usoni iwapo kutakuwa na idadi kubwa ya walipakodi.
“Sisi tunayo dhamira ya kuona viwango vya kodi vinapungua lakini haviwezi kupungua bila kuongeza wigo wa kodi, hivyo tunapaswa kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa kulingana na kipato chake kwa mujibu wa sheria” amesema Mwenda.

Amebainisha kuwa TRA itafungua vituo vya huduma za kodi vya kimkakati katika maeneo yote yenye mzunguko mkubwa wa biashara ili kuwezesha biashara, kurahisisha ulipaji kodi kwa hiari na kusogeza huduma za kodi karibu na wananchi huku akiagiza kila mkoa kuwa na vituo hivyo.
Akizungumza kuhusu kituo hicho Meneja wa mkoa wa Kodi Kinondoni Bw. Azizi Soka amesema kinatarajiwa kuhudumia walipakodi Zaidi ya 6790 kutoka Masaki, Msasani, Oyterbay, Bonde la Mpunga na maeneo ya jirani ambapo huduma zote za TRA zitapatikana kituoni hapo.
= = = = = = =








