Home Kitaifa TEKNOLOJIA YA AI: MWANGA MPYA KWA HUDUMA BORA ZA UMMA

TEKNOLOJIA YA AI: MWANGA MPYA KWA HUDUMA BORA ZA UMMA

Serikali imetangaza rasmi kuanza kwa matumizi ya Teknolojia ya Akili Mnemba (AI) katika utumishi wa umma, hatua inayotajwa kuwa mapinduzi makubwa katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi serikalini. Hatua hiyo inaashiria mwanzo wa enzi mpya ya matumizi ya teknolojia ya kisasa katika mifumo ya Serikali.

Akizungumza leo, Februari 12, 2026, jijini Dar es Salaam, katika mdahalo maalum ulioandaliwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi, amesema dunia inabadilika kwa kasi kubwa ya kiteknolojia na Serikali haiwezi kubaki nyuma katika mabadiliko hayo.

Amesema tangu uhuru, utumishi wa umma umepitia nyakati mbalimbali zenye changamoto na mahitaji yanayobadilika kulingana na wakati. Amekumbusha kuwa katika miaka ya 1990, Serikali ilifanya maboresho makubwa yaliyojumuisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Daudi ameeleza kuwa hatua ya sasa ya kuanza kutumia Akili Mnemba inalenga kurahisisha huduma, kupunguza urasimu na kuongeza uwazi katika taasisi za umma. Alisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yataongeza kasi ya utendaji na kusaidia kufanya maamuzi yanayotegemea takwimu sahihi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Ernest Mabonesho, amesema matumizi ya AI hayaepukiki katika dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa wa kiteknolojia. Alibainisha kuwa chuo hicho kina jukumu la kuwaandaa watumishi wa umma ili waweze kuendana na mabadiliko hayo.

Dkt. Mabonesho amesema mdahalo huo uliwakutanisha wadau kutoka sekta ya umma na binafsi kujadili namna bora ya kuijumuisha AI katika utendaji wa kila siku serikalini. Aliongeza kuwa mafunzo maalum yataendelea kutolewa ili kuhakikisha matumizi ya teknolojia hiyo yanafanyika kwa weledi na kwa kuzingatia usalama wa taarifa.

Baadhi ya washiriki wa mdahalo huo wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema kuwa AI itarahisisha utendaji kazi na kuongeza tija. Mjasiriamali Maiyolo Kalokola amesema awali alikuwa na hofu kuhusu teknolojia hiyo, lakini sasa ameona fursa kubwa iliyopo katika kuitumia kwa maendeleo.

Hata hivyo, wadau wameitaka Serikali kuweka mifumo madhubuti ya usalama wa taarifa na kutoa elimu ya kutosha kwa watumishi wa umma ili kuhakikisha matumizi ya AI yanakuwa na manufaa kwa taifa. Hatua hiyo imeelezwa kuwa msingi wa mageuzi mapya ya utumishi wa umma yanayolenga kutoa huduma bora, za haraka na zenye ufanisi zaidi kwa wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!