
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Serikali inaona umuhimu mkubwa wa taasisi ya ndoa kwani ndiyo msingi wa kuunda familia, raia wa taifa na hatimaye viongozi na askari wazalendo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Aprili 23, katika Kikao Kazi cha 15 cha Maafisa Utamaduni na Maafisa Maendeleo ya Michezo kutoka Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Prof. Kabudi aliwasilisha mada kuhusu Usimamizi wa Misingi ya Kitaifa inayojumuisha Maadili, Miiko, Umoja, Mshikamano na Uzalendo kupitia sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Prof. Kabudi ameeleza kuwa Serikali haiingilii mikataba yoyote ya kiraia kati ya watu au taasisi isipokuwa mkataba wa ndoa pekee, kwa kuwa familia inayozaliwa kupitia ndoa ndicho kiini cha taifa.
“Serikali inahusika na mkataba wa ndoa moja kwa moja, ni mkataba pekee ambao Serikali inausimamia. Hii ni kwa sababu familia ndio msingi wa raia wa taifa, na hao raia ndio wanakuwa viongozi, askari wazalendo. Ndiyo maana Serikali inaingilia mkataba huo,” alisisitiza Prof. Kabudi.
Aidha Prof. Kabudi amesema kwamba kwa mujibu wa taratibu za Serikali na mahakama, suala la talaka linazingatiwa pale ambapo wanandoa wamefikisha angalau miaka miwili ya ndoa.








