Home Kitaifa SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAONGEZA NGUVU ELIMU YA UFUNDI STADI KUCHOCHEA...

SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAONGEZA NGUVU ELIMU YA UFUNDI STADI KUCHOCHEA UCHUMI

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana leo Februari 16, 2025, katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mtumba jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Mzee Kasore, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mkazo mkubwa katika kuendeleza elimu ya ufundi stadi kama nguzo ya ajira, uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Akizungumza leo Februari 16,2026 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma,CPA  Kasore amesema VETA inaendelea kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kuifanya elimu ya ujuzi kuwa daraja la moja kwa moja kati ya vijana na ajira.

“Leo hatuzungumzii nadharia. Tunazungumzia maisha ya vijana kubadilika, ajira kuundwa na uchumi kujengwa kwa mikono ya Watanzania wenye ujuzi,” alisema.

VETA YAPANUA MTANDAO WA VYUO

CPA  Kasore amesema  kwa sasa VETA ina vyuo 80 vinavyohudumia zaidi ya wanachuo 86,000 kwa mwaka, huku Serikali ikiendelea na ujenzi wa vyuo katika wilaya 64 pamoja na chuo kimoja mkoani Songwe. Lengo ni kuhakikisha kila wilaya inakuwa na angalau chuo kimoja cha VETA.

Ameeleza kuwa ifikapo mwaka 2027, idadi ya vyuo inatarajiwa kufikia 152 na kuongeza udahili hadi wanafunzi 250,000 kwa mwaka.

MAGEUZI YA MFUMO WA UDAHILI

Katika kurahisisha upatikanaji wa mafunzo, VETA imeondoa mtihani wa mchujo (aptitude test), hatua iliyowezesha waombaji wote 18,875 wa mwaka huu kuchaguliwa kujiunga na mafunzo.

Aidha, wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu wanaojiunga na VETA wameondolewa baadhi ya masomo waliyokwisha soma ili kuhitimu kwa muda mfupi zaidi na kuongeza kasi ya upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi mahiri.

FURSA KWA WENYE MAHITAJI MAALUM NA MAFUNZO YA JIONI

CPA  Kasore amebainisha kuwa wanafunzi 195 wenye ulemavu wamefadhiliwa kikamilifu mafunzo yao ya muda mrefu mwaka huu. Pia, VETA imeanzisha mafunzo ya jioni (Evening Session) ili kuwapa nafasi wananchi walioko kazini au wenye majukumu ya asubuhi kujiendeleza.

MAFUNZO KWA NJIA YA MTANDAO – VSOMO

Katika kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia, VETA inaendesha mfumo wa mafunzo kwa njia ya kielektroni unaojulikana kama VSOMO, unaowezesha wanafunzi kujifunza nadharia kwa simu au kompyuta kabla ya kwenda chuoni kwa mafunzo ya vitendo.

Hadi sasa, zaidi ya wanafunzi 500 wamehitimu kupitia mfumo huo katika fani mbalimbali zikiwemo umeme, ufundi magari, upishi, urembo na ujasiriamali.

URASIMISHAJI UJUZI (RPL)

Kupitia mpango wa Urasimishaji Ujuzi (Recognition of Prior Learning – RPL), mafundi 25,523 wamerasimishiwa ujuzi wao hadi Januari 2026. Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, VETA imelenga kurasimisha mafundi 30,000 ikiwa ni sehemu ya Programu ya Mama Samia inayolenga kufikia vijana 80,000 ifikapo Juni 2027.

MIRADI YA USHIRIKIANO

VETA pia inatekeleza miradi mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, ikiwemo miradi ya kuwawezesha vijana na wanawake katika sekta za kilimo, ujasiriamali na ajira rasmi na zisizo rasmi.

CPA  Kasore amesisitiza kuwa dunia ya sasa inahitaji zaidi uwezo wa kufanya kazi kuliko vyeti pekee.

“Ujuzi ni mtaji, ujuzi ni ajira, ujuzi ni kujitegemea na ujuzi ni heshima,” amesisitiza.

WITO KWA VIJANA

Aidha amewahamasisha vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na VETA, akieleza kuwa uwekezaji unaofanywa na Serikali unaifanya taasisi hiyo kuwa injini ya kuzalisha ajira na kukuza uchumi shindani.

“Ninawaomba wanahabari muendelee kuwa mabalozi wa kuhabarisha jamii kuhusu fursa hizi. Kila kijana wa Tanzania anatakiwa kujua kuwa mustakabali wake uko mikononi mwake, na VETA ipo kumwezesha,” 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!