Home Kitaifa RAIS SAMIA KUZINDUA SERA YA TAIFA YA USIMAMIZI WA MNYORORO WA UGAVI...

RAIS SAMIA KUZINDUA SERA YA TAIFA YA USIMAMIZI WA MNYORORO WA UGAVI 2025

Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Alex Haraba,akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 4,2026 kuelekea uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025,unaotarajiwa kufanyika Aprili 8, 2026.

Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Alex Haraba (hayupo pichani) ,akizungumza na waandishi wa habari  kuelekea uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025,unaotarajiwa kufanyika Aprili 8, 2026. 

Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Alex Haraba (hayupo pichani) ,akizungumza na waandishi wa habari  kuelekea uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025,unaotarajiwa kufanyika Aprili 8, 2026.

Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Alex Haraba,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzungumza  na waandishi wa habari leo Aprili 4,2026 kuelekea uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025,unaotarajiwa kufanyika Aprili 8, 2026.

Na.Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI  inatarajia kuzindua  Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025, hatua inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika usimamizi wa rasilimali za umma nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 4,2026 jijini Dodoma, Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Alex Haraba, amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ataongoza uzinduzi rasmi wa sera hiyo Aprili 8, 2026 jijini Dodoma.

Bw. Haraba amesema kuwa uzinduzi wa sera hiyo ni hatua muhimu ya kimkakati inayolenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za serikali kupitia mnyororo wa ugavi.

 “Sera hiyo imeandaliwa kwa lengo la kuweka mfumo jumuishi na wa kimkakati wa kusimamia shughuli zote za mnyororo wa ugavi katika sekta ya umma. Mfumo huo unahusisha hatua mbalimbali kuanzia upangaji wa mahitaji, ununuzi wa umma, ugomboaji na uondoshaji wa mali za serikali, upokeaji na urejeshaji wa bidhaa au vifaa, uhifadhi na utunzaji, matumizi, usambazaji hadi uondoshaji wa mali za umma.”amesema Bw.Haraba

Kupitia sera hiyo, Serikali inalenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma. Aidha, inalenga kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi unazingatia ubora unaotakiwa, unapatikana kwa wakati na kwa thamani halisi ya fedha (Value for Monye).

Aidha Bw.Haraba amesema kwa muda mrefu shughuli za mnyororo wa ugavi zimekuwa zikitekelezwa kupitia sheria,kanuni na mifumo mbalimbali ya kiutendaji bila kuwa na mwongozo mmoja wa kisera unaounganisha hatua zote kwa mtazamo na jumuishi.

“Kutungwa kwa sera hii kunalenga kufungamanisha shughuli hizo ili kuimarisha uratibu na usimamizi jumuishi wa shughuli za mnyororo wa ugavi,kuboresha matumizi na usimamizi wa rasilimali za umma pamoja na kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu ya serikali.”amesisitiza

Amesema kwa kuzingatia  sehemu kubwa ya matumizi ya serikali kupita katika shughuli za ununuzi wa umma, mnyororo wa ugavi ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha rasilimali za umma zinasimamiwa kwa ufanisi, zinachochea ukuaji wa uchumi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Vilevile, sera hiyo inaweka mkazo katika kuimarisha utawala bora, matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa mnyororo wa ugavi, na ushiriki wa sekta binafsi. Pia inalenga kuimarisha ushiriki wa makundi maalum ya kijamii ili kupanua wigo wa fursa za kiuchumi na ajira kwa Watanzania.

Katika hatua nyingine, sera inahamasisha matumizi ya rasilimali na malighafi za ndani katika uzalishaji wa bidhaa na huduma ili kuongeza thamani ya rasilimali za nchi, kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani na kuimarisha ushindani wa uchumi wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Amesema kuwa Mwelekeo huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi imara, shindani na jumuishi unaoongeza thamani ya rasilimali za ndani na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, biashara na maendeleo ya taifa.

Serikali inatarajia kuwa utekelezaji wa sera hiyo utaimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, kuongeza ufanisi katika miradi ya maendeleo, kupunguza upotevu wa rasilimali na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hata hivyo Wananchi wametakiwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa sera hiyo kwa kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma, ili kuhakikisha manufaa yake yanafika kwa Watanzania wote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!