Na Shomari Binda, Musoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof.Sospeter Muhongo ameahidi kuchangia saruji na mabati kwenye ujenzi wa shule ya sekondari Nyasaungu.
Ahadi hiyo ameitoa wakati alipotembelea Kijiji cha Nyasaungu kilichopo pembezoni mwa jimbo hilo ili kuona shughuli za kimaendeleo.
Katika ziara hiyo Muhongo ameona dhamira ya wananchi wa Kijiji hicho katika kutaka kufungua sekondari yao januari mwakani na kuamua kuwaunga mkono.
Miradi inayotekelezwa kwenye kijiji hicho ni ujenzi wa sekondari, ujenzi wa zahanati pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya elimu kwenye shule ya msingi Nyasaungu.
Katika kikao na wananchi hao, kero zilizotolewa na kupata majibu kutoka kwa mbunge huyo ni kuhusu upungufu mkubwa kwenye upatikanaji wa maji, umeme, hali ya chakula kutokana na ukame pamoja na upungufu wa walimu kwenye shule ya msingi Nyasaungu.
Muhongo amesema Kata ya Ifulifu haikuwa na eekondari yake na kuishukuru serikali kuchangia kwa kiasi kikubwa sana ujenzi wa sekondari ya Kata ya Ifulifu inayojengwa Kijiji cha Kabegi.
Amesema Kijiji cha Nyasaungu ni moja ya vijiji vitatu vya Kata ya Ifulifu ambacho kipo pembezoni na mbali na vijiji vingine vya Kata na kukifanya kuwa na ugumu wa kufikika hasa wakati wa mvua na mazingira hayo ni hatarishi kwa wanafunzi.
Aidha Muhongo ameiomba halmashauri ianze kuchangia ujenzi wa Sekondari hiyo ambbayo watumiaji wake wengi watakuwa watoto wa wafugaji wa Kijiji cha Nyasaungu.
Ujenzi umefikia hatua ya kukamilisha vyumba 3 vya madarasa,choo cha matundu 6 pamoja na jengo la utawala.
Kwa sasa jimbo la Musoma vijijini linajenga sekondari 4 mpya ambazo ni Nyasaungu sekondari iliyopo Kata ya Ifulifu, sekondari ya pili ya Muhoji Sekondari Kata ya Bugwema, Wanyere sekondari
Kata ya Suguti na sekondari ya Kisiwa cha Rukuba Kata ya Etaro.









