Home Kitaifa MKENDA: ELIMU YA MSINGI KUPUNGUZWA HADI MIAKA SITA KUANZIA 2027/2028

MKENDA: ELIMU YA MSINGI KUPUNGUZWA HADI MIAKA SITA KUANZIA 2027/2028

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda,akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo elekezi ya Wathibiti Ubora wa Shule ngazi ya wilaya uliofanyika   wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani.

……

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema kuwa jukumu kubwa la Wathibiti Ubora wa Shule ni kuhakikisha utekelezaji wa sera, sheria, miongozo na mikakati ya elimu unafanyika kwa ufanisi.

Akizungumza  wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani katika ufunguzi wa mafunzo elekezi ya Wathibiti Ubora wa Shule ngazi ya wilaya, ameeleza kuwa watendaji wanapaswa kusaidia katika utekelezaji wa sera na kuhakikisha wanazielewa kikamilifu, hususani zinazohusu elimu ya amali na elimu ya lazima.

Profesa Mkenda amesema wathibiti Ubora wa Shule wanapaswa kutoa taarifa juu ya changamoto zinazojitokeza shuleni ikiwemo ukosefu wa vifaa au madarasa kwa Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya ili hatua za kutatua changamoto hizo zichukuliwe haraka.

Akizungumzia mageuzi makubwa ya Sekta ya Elimu, Waziri amesema kuwa kuanzia mwaka wa masomo 2027/2028, elimu ya msingi itaanza kutolewa kwa Miaka Sita badala ya Saba na elimu ya lazima itakuwa miaka kumi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.

“Mabadiliko haya yataleta “double cohort,” ambapo wanafunzi wa darasa la saba (mfumo wa zamani) na darasa la sita (mfumo mpya) wataingia kidato cha kwanza kwa wakati mmoja. Hata hivyo, hali hiyo ni ya mpito na mfumo utarejea katika “single cohort” baada ya muda,’amefafanua Waziri Mkenda.

Amesema Serikali inawekeza katika shue za ufundi, lakini bado kuna uhaba wa karakana, vifaa na walimu wenye sifa huku akisisitiza Halmashauri kupanga bajeti kwa umakini ili kuzuia shule kufungwa kutokana na ukosefu wa mahitaji ya msingi.

Mkurugenzi Msaidizi wa Uthibiti Ubora wa Shule, Monica Mpululu, amesema kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kasi na kwa ushirikiano wa karibu na Wathibiti Ubora wa shule nchini.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa wizara imeendelea kuwawezesha wathibiti Ubora wa shule kwa kuwapatia rasilimali muhimu, ikiwemo fedha na vifaa vya kazi ambayo inasaidia kuboresha usimamizi na ufuatiliaji wa shule katika maeneo mbalimbali ya nchi na
kuongeza ufanisi wa kazi za uthibiti ubora.

Mpululu amesema kuwa ushirikiano wa wadau wote wa elimu ni msingi wa mafanikio ya sekta, na kwamba juhudi zinazofanywa sasa ni matokeo ya kazi ya pamoja inayolenga kuinua kiwango cha elimu kwa manufaa ya taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!