Home Kitaifa MIKATABA YA TRILIONI 1.2 YASAINIWA NA REA KUSAMBAZA UMEME VITONGOJI 9,009 NCHINI.

MIKATABA YA TRILIONI 1.2 YASAINIWA NA REA KUSAMBAZA UMEME VITONGOJI 9,009 NCHINI.

Na Deborah Lemmubi-Dodoma.

Waziri wa Nishati Mhe Deogratius Ndejembi amesema kuwa upatikanaji wa Umeme kwa Watanzania wote ni agenda ya Kitaifa na ya kimkakati na kwamba Serikali itaendelea kuwekeza pamoja na kuboresha mazingira kwa kuwapatia nishati safi na kuwa chachu ya maendeleo endelevu.

Waziri Ndejembi amesema hayo leo Jijini Dodoma Januari 17,2026 katika hafla fupi ya Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambayo imesaini mikataba 30 yenye thamani ya shilingi Trilioni 1.2 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme katika Vitongoji 9,009 utakaonufaisha Wateja wa awali 290,300 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara.

Aidha amesema kuwa kusaini kwa mikataba ya Mradi huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha ifikapo 2030 vitongoji vyote nchini viwe vimekwisha fikiwa na nishati ya umeme.

Upatikanaji wa umeme kwa wote ni agenda ya Kitaifa na ya kimkakati,Serikali itaendelea kuwekeza,kusimamai na kuboresha mazingira kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwapatia nishati safi ya kupikia na kuwa chachu ya maendeleo jumuishi na endelevu”.

Serikali imedhamiria kuhakikisha hakuna Mtanzania atakayebaki bila umeme. Tumekamilisha vijijini na sasa ni zamu ya vitongoji na kwa mikataba hii iliyosainiwa hivi leo ni ushahidi wa dhamira hiyo ya Serikali“.

Pia amebainisha kuwa kati ya mikataba hiyo 30 iliyosainiwa, mikataba 21 ni ya kampuni za Wazawa na mikataba mingine tisa ni ya kampuni kutoka Nje ya nchi ambazo zimesajiliwa hapa nchini.

Na kuongeza kuwa Serikali ya Rais Samia inatambua Sekta ya Nishati ni injini ya kuchochea maendeleo na amekuwa akitoa fedha nyingi ili kuboresha maisha ya Wananchi wa vijijini.

Pamoja na hayo pia ameipongeza REA kwa kuendelea kuwa chombo imara cha Serikali kwa utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya kusimamia na kupeleka nishati bora kwa Wananchi kwa kuendelea kuhakikisha kuwa Taasisi zote za Umma zinaunganishwa na umeme zikiwemo shule za msingi, sekondari na vituo vya afya.

Awali akitoa salamu Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amesema Serikali itaendelea na kasi yake ile ile ya kusambaza umeme ili kuleta tija inayokusudiwa.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu amepongeza jitihada mbalimbali za REA katika kutimiza azma ya Serikali ya kuhakikisha nishati ya umeme inasambaa kote nchini.

Hongereni REA mnafanya kazi kubwa, leo hii tumefurahi kushuhudia tukio la kihistoria la kusaini mikataba ya kusambaza umeme vitongojini”.

Akizungumzia utekelezaji wa Miradi mbalimbali, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema kuwa REA inatekeleza azma ya Serikali ya kuhakikisha umeme unawafikia Wananchi kwa vitendo.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2025, Serikali imefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara. Hatua hii imeleta mapinduzi ya kweli ya kiuchumi na kijamii, ikichangia kuboresha maisha ya Wananchi wanaoishi vijijini”.

Amesema mwaka 2021 kati ya vitongoji 64,359 vilivyopo Tanzania Bara, vitongoji 28,258 pekee vilikuwa na umeme wakati vitongoji 36,101 vilikosa huduma hiyo muhimu.

Na kusema kuwa kupitia utekelezaji wa Miradi mbalimbali kuanzia mwaka 2021 hadi Desemba 2025, Serikali imeunganisha umeme katika vitongoji 10,745, na hivyo kuongeza idadi ya vitongoji vyenye umeme kufikia 39,003.

Aidha, amesema vitongoji 2,435 vipo katika hatua za utekelezaji wa miradi inayoendelea na hivyo kufanya jumla ya vitongoji 41,438
kuwa tayari vimeunganishwa au vipo katika utekelezaji.

Amesema Mradi utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na kuwasisitiza Wakandarasi kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya rushwa na tabia zisizo na maadili.

Mradi huu wa Umeme huu utasambazwa katika Mikoa 25 ya Tanzania Bara ikiwemo Mkoa wa Tanga kwa vitongoji 527 na umepata Shilingi Bilioni 73.7,Tabora vitongojo 660 na umepata Shilingi Bilioni 109.3 na Songwe vitongoji 173 ma umepata Shilingi Bilioni 28.7.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!