
Wenyeji wa mchezo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (NBC), JKT Tanzania, walijikuta katika wakati mgumu baada ya kuchapwa mabao 2-1 na wekundu wa Msimbazi, Simba SC, katika mtanange uliochezwa Novemba 8 katika Dimba la Meja Jenerali Isamuyo, Jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, JKT Tanzania walitangulia kupata bao la uongozi katika dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza cha mchezo huo.
Hata hivyo, Simba ilionesha makucha yake mithili ya mnyama aliyejeruhiwa, ambapo Edward Songo aliifungia timu hiyo bao la kusawazisha katika dakika ya 60 ya mchezo huo.
Mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah, alipigilia msumari wa pili uliowezesha Simba kumaliza dakika 90 kwa ushindi na kupata alama tatu muhimu, hivyo kuifanya timu hiyo kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa alama 9 baada ya kushinda mechi tatu mfululizo.








