
Tume ya Ushindani (FCC) imetangaza mkakati wa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Mlaji Duniani, kwa lengo la kuhakikisha walaji wanapata bidhaa na huduma salama zinazokidhi viwango vinavyotakiwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema tume hiyo itaendelea kulinda maslahi ya walaji na kuimarisha ushindani wa haki sokoni ili kujenga mazingira bora ya biashara.

Ameeleza kuwa Siku ya Mlaji huadhimishwa kila mwaka Machi 15, huku kilele chake kikiwa Machi 31. Mwaka huu maadhimisho yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Bidhaa Salama, Imani kwa Mlaji,” inayosisitiza umuhimu wa usalama na ubora wa bidhaa na huduma sokoni.
Ngasongwa amesema maadhimisho hayo ni fursa ya kujenga imani ya walaji kwa kuimarisha uwazi, ubora na uwajibikaji miongoni mwa wafanyabiashara, hali inayochochea ushindani wa haki na ukuaji wa uchumi.
Katika kuadhimisha siku hiyo, FCC imepanga kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ili kuongeza uelewa wa haki za mlaji na umuhimu wa ushindani wa haki, huku ikiwasihi wazalishaji, wasambazaji na watumiaji kushirikiana kujenga soko lenye kuzingatia maslahi ya mlaji.








