
Na Boniface Gideon, TANGA
MKUU wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt.Batilda Buriani amesema Serikali mkoani humo kupitia Wakala wa Usambazaji Maji vijijini na Usafi wa Mazingira ‘RUWASA’,imeanzisha mkakati wa kupanda miti inayoendana na utunzaji wa vyanzo vya Maji ili kuongeza kiwango cha uzarishaji maji,
Batilda amesema,Jumuia zote za watumia Maji (CBWSO ) zitakuwa na kazi ya kusimamia Wananchi na wadau mbalimbali wa mazingira kupanda miti kwanjia ya vitalu vya miti ambayo itapandwa karibu na vyanzo vya Maji ili kuweza kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Dkt Buriani ameyasema hayo leo Novemba mosi wakati wa hafla kukabidhi gari lenye thamani ya Mil.154 pamoja na pikipiki mbili zilizotolewa na wizara ya maji ambazo zimegharimu kiasi cha shilingi Million 4 ,ambazo zitakwenda kutumiwa na watumishi wa RUWASA katika Wilaya za Pangani na Korogwe kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wao sambamba na kuendelea kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

“Kama tunavyojua sera ya Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndio kichwani, vyombo hivi vinakwenda kuendelea kuhakikisha hakuna changamoto ya upatikanaji wa maji na kufikia adhima ya Serikali ya kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini ifikapo 2025”
“Lakini pia wizara imetuletea pikipiki mbili zinazokwenda kwa vyombo vya jumuiya za watumiaji wa maji ‘CBWSO’ za Mkombozi wilayani Pangani na Mwakipokwa iliyoko Korogwe kwaajili ya kwenda kuboresha upatikanaji wa maji katika vijiji vyetu”Amesema Dkt.Buriani
“Tumekubaliana kwamba Tanga ya kijani inawezekana tumeanza mikakati mahususi ya kuendelea kutumia wadau wetu wote kupanda miti tukitumia utaalam wa wenzetu wa Wakala wa Misitu Tanzania ‘TFS’ ili tuweze kupanda miti sahihi kwa sababu mara nyingi tumekuwa tukipanda miti ambayo inakindhana na hali ya hewa tunataka miti ambayo itasaidia mazingira”
“Tumekubaliana na viongozi wa jumuiya za watumika Maji na tumesisitiza miche iwe karibu na Wananchi ili tukianzisha zoezi la upandaji wa miti tuweze kupanda kwa pamoja meneja wa mkoa ulisimamie hilo ili ionekane kwamba kweli hili ambalo tumekubaliana kwenye mikutano liweze kutimia” alisisitiza Dkt. Buriani.
Meneja wa Wakala wa Maji vijijini ‘RUWASA’ mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo amesema kuwa kupatikana kwa vyombo hivyo vya usafiri kwa Wilaya za Pangani na Korogwe kunawapa motisha ya utendaji kazi watumishi ambao wanapambana kuhakikisha huduma ya maji kwa wananchi inaimarika.
“Pikipiki hizi pamoja na gari hili vinakwenda kuboresha utoaji huduma kwa wananchi kuwafikia kule waliko lakini kikubwa zaidi mazingira ya utendaji kazi yanaenda kuimarika na hivyo huduma ya maji inaendelea kuimarika katika wilaya ya Pangani na Korogwe katika vyombo vya Maji”
Kufuatia tamko la Mkuu wa Mkoa wa Tanga,juu ya kuwasimamia Wananchi walioko katika jumuia za watumia Maji ngazi ya jamii ‘CBWSO’ Mhandishi Lugongo amesema “Suala la upandaji wa miti kwa ngazi za watumia maji na CBWSO zote kuwa na vitalu vya upandaji miti sisi kama watumishi tumelipokea na tunaenda kulisimamia kwa kushirikiana na viongozi wote na itakapofika wakati wa kupanda basi tuweze kigawa miche kwa wananchi na mazingira yetu yaendelew kuwa salama lakini kikubwa zaidi tunakwenda kuhifadhibvyanzo vya maji”
Katibu wa jumuiya za watumia Maji Wilaya ya Korogwe Mhandisi Kapota Abdi Kapota alisema kuwa suala la utunzaji wa vyanzo vya Maji ni la kila mwananchi ili kuendelea kukabiliana uharibifu wa vyanzo vya Maji ambao unaweza kupelekea changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi.
“Pamoja na majukumu ya kusimamia jumuia za watumia Maji lakini tuna kazi ya kuhakikisha tunatunza vyanzo vya Maji na hii tunakwenda kutekeleza agizo la kuhakikisha kila CBWSO zilizoko mkoa wa Tanga zinaanzisha vitalu vya miti kwa kuwashitikisha Wananchi katika utunzaji wa mazingira” alisema Mhandisi Kapota.

MWISHO.