Home Kitaifa CAMARTEC YABUNI TEKNOLOJIA MPYA KUINUA SEKTA YA KILIMO NA UFUGAJI

CAMARTEC YABUNI TEKNOLOJIA MPYA KUINUA SEKTA YA KILIMO NA UFUGAJI

Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) kimeanzisha mbinu mpya za mafunzo kwa wakulima kuhusu usindikaji wa mazao, ikiwemo mwani korosho na vyakula vingine, ili kuhakikisha wakulima wanapunguza hasara wanaposafirisha bidhaa zao sokoni, huku teknolojia hiyo ikiongeza muda wa kukaa kwa bidhaa bila kuharibika.

Vilevile, Katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa malisho inayowakabili wafugaji wengi nchini, kituo hicho kimebuni teknolojia ya kuchakata mabua ya mahindi na magunzi kwa ajili ya kutengeneza chakula cha mifugo ili kunusuru mifugo dhidi ya athari za ukame, ambao umekuwa ukisababisha hasara kubwa ya kiuchumi kwa wafugaji kutokana na vifo na kupungua kwa tija ya mifugo yao.

Hayo yamesemwa Januari 19, 2026 na Naibu Waziri Dennis Londo alipotembelea kituo hicho na kukiagiza kuongeza kasi ya ubunifu ili kumwondoa mkulima katika matumizi ya jembe la mkono na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Aidha, alisema pamoja na Mafanikio kilichonacho ni muhimu kwa kituo hicho kutafuta wabia katika halmashauri mbalimbali nchini ili kuhakikisha zana hizo zinazalishwa kwa wingi na kuwafikia wananchi vijijini na kuibadili sekta ya kilimo kuwa fursa ya kibiashara

Waziri Londo pia aliongeza kuwa ukosefu wa teknolojia rafiki unasababisha matumizi ya ardhi kubwa kuzalisha mazao machache, hivyo CAMARTEC inapaswa kuhakikisha teknolojia zao zinawafikia wakulima ili wajikwamue kiuchumi.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CAMARTEC, Mhandisi Godfrey Mwinama, alieleza kuwa kituo kimeanzisha mashamba darasa ili kuwawezesha wakulima kujifunza kwa vitendo matumizi ya zana bora kama mashine za kuchanjua mahindi, matrekta ya kisasa, na teknolojia za usindikaji zinazorahisisha kazi za shambani.

Aidha, CAMARTEC imeweka nguvu kubwa katika uzalishaji wa mitambo ya kubangua korosho kwa ajili ya wakulima wa mikoa ya Lindi, Mtwara, na maeneo mengine yanayozalisha zao hilo ili kuongeza thamani katika mnyororo wa zao la korosho na kuwasaidia wakulima kupata soko la uhakika na bei nzuri zaidi kuliko kuuza zao ghafi.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango, Audax Bahweitama, alihimiza kituo hicho kuhakikisha kuwa zana zote zinazobuniwa zinauzwa kwa bei nafuu na inayohimilika kwa mkulima mdogo. Alieleza kuwa upatikanaji wa zana hizo maeneo ya vijijini utachochea ukuaji wa uchumi wa taifa na kuongeza mapato ya serikali kupitia mnyororo wa thamani unaoanzia shambani hadi viwandani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!