Home Kitaifa BARAZA LA WAFANYAKAZI WIZARA YA ELIMU LAWEKA MIKAKATI YA UTEKELEZAJI ENDELEVU

BARAZA LA WAFANYAKAZI WIZARA YA ELIMU LAWEKA MIKAKATI YA UTEKELEZAJI ENDELEVU

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, leo Februari 12, 2026, amefungua rasmi Baraza la 36 la Wafanyakazi wa Wizara hiyo lililofanyika jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa baraza hilo, Prof. Mkenda amewapongeza viongozi na watumishi wa wizara kwa hatua mbalimbali walizochukua katika utekelezaji wa majukumu yao, huku akisisitiza kuongeza kasi katika utekelezaji wa mipango iliyopo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Amesema kuwa mipango na makadirio ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027 yanapaswa kuakisi kikamilifu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, hususan katika eneo la elimu ya lazima ya miaka 10.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha Mpango wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kwa watoto wa elimu ya awali pamoja na wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili.

Prof. Mkenda pia amegusia Mpango wa Pamoja wa Ushirikiano kati ya Vyuo na Viwanda, akieleza kuwa ni muhimu katika kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema Baraza la Wafanyakazi hufanyika mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ustawi wa wizara pamoja na tathmini ya utekelezaji wa majukumu yake.

Awali, Kaimu Katibu wa Baraza hilo kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bi. Suzana Lushinge, amesema kuwa lengo la baraza hilo ni kutathmini utekelezaji wa mipango ya wizara pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi husika.

Aidha, ametoa rai kwa menejimenti ya wizara kuendelea kushirikiana kwa karibu na watumishi ili kuhakikisha majukumu yaliyopangwa yanatekelezwa kwa ufanisi na weledi mkubwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!