
Na Deborah Lemmubi-Dodoma.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Ajira,Vijana na wenye Ulemavu Mhe Ridhiwani Kikwete amesema kuwa katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi,kuwa pamoja na mambo mengine itaadhimishwa kauli mbiu ya nafasi ya akili unde na Teknolojia za Kidigitali katika mapinduzi ya usalama na afya kazini ikiwa inalenga kuhamasisha na kuwakumbusha Waajiri kujiandaa kutumia Teknolojia hiyo katika uzalishaji na utoaji wa huduma bora.
Waziri Kikwete ameyasema hayo Wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo hii Aprili 23,2025 Jijini Dodoma kuhusu maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika Mkoani Singida Aprili 28,2025.
Na kusema lengo la Maadhimisho hayo ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha uwekaji wa mazingira salama mahali pa kazi.
“Teknolojia hii inaenda kuleta mabadiliko chanya ikiwemo mashine na mifumo inayotumia akili unde kufanya kazi kwa haraka,kwa usahihi bila kuchoka,ni vyema pia kutambua kuwa matumizi hayo hayamaanishi kupoteza ajira bali kuleta mabadiliko katika ajira”.
Na kuongeza kuwa matumizi ya Teknolojia hiyo yataongeza mahitaji ya wataalam, mafundi wa mitambo ya kisasa na wasimamizi wa taarifa na mifumo ya akili unde.
Aidha akizungumzia namna maadhimisho hayo yatakavyofana amesema, yataambatana na maonesho ya usalama na afya mahala pa kazi na wadau wengine ili kutoa elimu kwa umma na kubadilishana uzoefu miongoni mwao juu ya masuala mbalimbali ya usalama.
“Maonesho haya yatafanyika viwanja vya Mandewa -Singida ambapo pia Kutakuwa na kliniki ya uchunguzi wa afya za wafanyakazi kwenye magonjwa ya wanawake, afya ya akili, sukari, saratani na macho“.
Katika Maadhimisho hayo pia Waziri Kikwete ndiye anayetarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.








