Home Kitaifa AFYA MSINGI WA MAENDELEO YA UCHUMI

AFYA MSINGI WA MAENDELEO YA UCHUMI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amesema afya ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi ya taifa, akisisitiza kuwa wananchi wenye afya njema wana mchango mkubwa katika shughuli za uzalishaji na ujenzi wa uchumi.

Akizungumza leo Jumatatu Januari 19, 2026, katika Jukwaa la Uwekezaji wa Viwanda vya Dawa Tanzania jijini Dar es Salaam, Dkt. Shekalaghe amesema serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vya kutosha ili wananchi wapate huduma za matibabu kwa wakati na kurejea katika shughuli za maendeleo.

Ameeleza kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya na imejikita katika kuhimiza uwekezaji wa ndani na wa kimataifa ili kufikia lengo la kujitegemea katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba. Aidha, amempongeza Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, kwa kuchukua hatua za haraka tangu Desemba 23, 2025, ikiwemo kuanzisha Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji wa Dawa.

Dkt. Shekalaghe amesema wizara imefungua fursa kwa wawekezaji kuonesha nia ya kuwekeza kupitia tovuti yake, hatua inayolenga kurahisisha na kuharakisha taratibu za uwekezaji. Ameongeza kuwa mwitikio mkubwa wa washiriki katika jukwaa hilo unaonesha utayari wa wadau kushirikiana na serikali kufanikisha uzalishaji wa bidhaa za afya ndani ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!