Home Kitaifa WANANCHI WASIKITISHWA KUAMBIWA WAVAMIZI WA ENEO WALILOISHI ZAIDI YA MIAKA 70 ILIYOPITA...

WANANCHI WASIKITISHWA KUAMBIWA WAVAMIZI WA ENEO WALILOISHI ZAIDI YA MIAKA 70 ILIYOPITA MANISPAA YA MUSOMA

Na Shomari Binda-Musoma

WAKAZI wa eneo la mtaa wa Baruti Kata ya Nyakato manispaa ya Musoma wamesikitishwa kuitwa wavamizi kwenye eneo waliloishi zaidi ya miaka 70 iliyopita.

Wakizungumza kwenye kikao kilicho kilichowashirikisha wakazi hao na maafisa ardhi kutoka halmashauri ya manispaa ya Musoma na kamishina wa ardhi wa mkoa wa Mara wamesema suala hilo limewasikitisha.

Wakazi hao wamesema katika kipindi chote cha uongozi wa serikali kuanzia awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere hawajawahi kuambiwa wavamizi hadi awamu hii ya 6.

Kwenye kikao hicho wakazi hao wamesema yapo maeneo ya shughuli za serikali ambayo yamezungushiwa uzio miaka yote na wao wakiishi kama majirani na kushangazwa kuitwa wavamizi.

Mmoja wa wakazi hao, Mikidadi Mahebwa ambaye amezaliwa na kuishi katika eneo hilo zaidi ya miaka 70 iliyopita hadi kufanyika kikao hicho ,alishangaa kuambiwa wao ni wavamizi wa eneo la wakala wa hifadhi ya taifa ya chakula (NRFA) ambao walipimiwa eneo hilo mwaka 1969.

Amesema hawana hati ya eneo hilo na wamekuwa wakisubili urasimishaji kwa muda wote ili waweze kupata hati na kushangazwa kuambiwa wavamizi

Aidha Afisa Ardhi wa manispaa ya Musoma Anicas Vilumba alidai kuwa kiwanja chenye mgogoro ni eneo la NRFA ambalo kwa sasa ndiyo wanataka kuwatayalishia hati kama serikali ilivyoelekeza.

Kutokana na hatua hiyo wakazi hao wanashangazwa kwa nini NRFA wamilikishwe eneo lao leo mwaka 2023 likiwa na nyumba zao bila kulipwa fidia.

Kaimu Kamishina Afisa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mara, Dickson Mwinuka amesema wamefika eneo hilo ili kuangalia na kuona mipaka yake na wanakwenda kulifanyia kazi.

Amesema wakazi hao wasiwe na wasiwasi kwa kuwa wametembelea eneo husika wanakwenda kukaa na kulipatia ufumbuzi na kumaliza mgogoro huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!