
Wananchi mkoani Tabora wamehimizwa kujiunga na huduma ya umeme na kukumbatia matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo majiko ya umeme, ili kulinda afya zao, kutunza mazingira na kuboresha maisha ya kila siku.
Rai hiyo imetolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia ziara ya kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuhusu miradi ya nishati vijijini mkoani humo.

Kupitia ziara hiyo, wananchi wanapatiwa elimu kuhusu taratibu za kuomba na kuunganishiwa huduma ya umeme, matumizi sahihi na yenye tija ya nishati hiyo, pamoja na tahadhari za kiusalama wanazopaswa kuzingatia wanapotumia umeme majumbani na katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Aidha, REA imewahimiza wananchi kutumia nishati safi ya kupikia ili kupunguza matumizi ya nishati chafu, ambayo huchangia uchafuzi wa mazingira na kuwaweka watumiaji katika hatari ya kupata matatizo ya kiafya kutokana na moshi.

Matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo umeme, yanaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, hivyo kuchangia uhifadhi wa mazingira na kuboresha afya za familia.
Vilevile, wananchi wametakiwa kushiriki katika kutunza miundombinu ya umeme na kuzingatia usalama wakati wa matumizi yake ili kuhakikisha huduma hiyo inaendelea kupatikana kwa uhakika.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za REA kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma za nishati vijijini na kuwahamasisha kutumia nishati kwa usalama, ufanisi na kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira.









